Utata Ajali Ya Basi Ikiua Watu 12, Dereva Asimulia

Wakati Jeshi la Polisi mkoani Dodoma wakiumiza vichwa kuhusu idadi ya abiria waliokuwamo kwenye basi la Frester, wadau wameeleza ufinyu wa barabara ya Dodoma-Dar es Salaam huenda ukawa chanzo cha ajali za mara kwa mara.

Hii ni ajali ya pili kutokea ndani ya siku nne baada ya ile ya Februari 4 iliyotokea wilayani Korongwe Mkoa wa Tanga, iliyosababisha vifo vya watu 20.

Ajali hiyo ilihusisha gari aina ya Coaster iliyokuwa imebeba maiti iliyokuwa ikisafirisha kwenda kuzikwa mkoani Kilimanjaro.


Katika ajali hiyo, watu wanane walifariki dunia papo hapo na wengine 12 walifariki dunia wakati wakipatiwa matibabu hospitalini.


Wadau wafunguka

Wasomi, wafanyabiashara na wananchi wameshauri Serikali ianze kuona umuhimu wa kuzitanua barabara zake kuu.

Diwani wa Buigiri wilayani Chamwino alisema barabara nyingi ni nyembamba, hivyo ajali za uso kwa uso haziwezi kuepukika kama barabara hizo hazitarekebiswa.

“Nashauri barabara hii ipanuliwe na ziwekwe alama za barabarani kwa sababu watoto wetu wanagongwa kila mara,” alisema.

Mfanyabiashara Rajabu Athumani alisema kuna haja ya kuboresha miundombinu ya barabara, kwani barabara nyingi zinaonekana kuchakaa na kusababisha ajali. Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha St John cha jijini Dodoma, Dk Shadidu Ndossa alisema kuna haja ya kuwekeza katika teknolojia kwa kufunga kamera za barabarani.

“Ni gharama, lakini inasaidia kuokoa maisha ya watu, nchi kama Rwanda kuna kamera zenye kujiendesha zenyewe, zimesaidia kupunguza ajali barabarani,” alisema.

Pia alisema njia nzuri ya kumwadhibu binadamu ni kuchukua kipato chake hivyo kuna haja ya faini kuongezwa.


Mkanganyiko idadi ya abiria

Kuhusu idadi ya abiria, ni swali lililomshtua Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Martin Otieno alipozungumza na Mwananchi, kwani ajali hiyo ilisababisha vifo 10 papo hapo na majeruhi wawili waliofia hospitali huku ikiacha majeruhi 63 (wanaume 40 na wanawake 23).


Idadi hiyo ikijumlishwa inafanya jumla ya abiria waliokuwa kwenye basi kuwa 75 wakati uwezo wa basi ni kubeba abiria waliokaa 55 hadi 60. Hakuna taarifa za waliokuwamo kwenye lori.

Ajali hiyo ambayo ilitokea usiku wa kuamkia jana katika kijiji cha Silwa Kata ya Pandambili wilayani Kongwa iliyohusisha basi la Frester lilokuwa likitokea mkoani Kagera kuelekea Dar es Salaam, liligongana na lori lilokuwa likielekea Dodoma.

Alisema ni suala la kufuatiliwa; “lakini kati ya maiti hizo zipo za watoto wachanga ambao huwa wanabebwa na wazazi wao.”

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma,Dk Ernest Ibenzi alisema kati ya majeruhi 15 waliofikishwa katika hospitali hiyo wawili wapo wodi ya wagonjwa mahututi.


Dereva asimulia

Akisimulia kwa shida huku akiwa amefungwa bandeji kichwani na mkononi akiwa wodi namba moja katika hospitali ya Rufaa Mkoa wa Dodoma, dereva wa basi hilo, Enock Martin alisema ajali hiyo ilitokea saa 7:20 usiku.

Alisema wakati ajali inatokea mvua ilikuwa inanyesha na alitaka kulipita gari lilokuwa limepaki nje kidogo ya barabara, kumbe mbele kulikuwa na lori lilokuwa limebeba mifuko ya saruji.

“Ndiyo tukagongana uso kwa uso, baada ya ajali sikuona chochote mpaka nilivyofikishwa hapa hospitalini,” alisema dereva huyo.


Asimulia alivyojiokoa

Majeruhi Abdulkarim Cyprian ambaye ameumia sehemu za kichwani alisema alipanda basi hilo eneo la Iborogero mkoani Tabora na walipofika Dodoma gari liliharibika, hivyo walienda gereji kwa ajili ya matengenezo. “Namshukuru Mungu kwa kutoka salama...wakati ajali inatokea nilikuwa macho, wengi walikuwa wamelala.


Alisema baada ya kutoka akiwa na mwenzake walianza kuwaokoa wenzao waliokuwa wamelaliwa na mifuko saruji iliyokuwa katika lori na ilipofika saa tisa usiku watu walianza kufika eneo hilo na kuanza kupelekwa hospitalini.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments