Uvuvi wa dagaa Ziwa Victoria wasitishwa


 Shughuli za uvuvi wa dagaa katika mialo ya Mkoa wa Mwanza zimesitishwa kwa siku 15 kuanzia Januari 24, mwaka huu kutoa fursa samaki hasa dagaa kuzaliana katika kipindi cha mbalamwezi.

Uamuzi huo ni kwa mujibu wa sheria na kanuni za uvuvi na marekebisho yake ya 2020 na kwa mujibu wa Kaimu Ofisa Mfawidhi Ulinzi na Usimamizi wa Rasilimali za Uvuvi Kanda ya Ziwa, Laurent Mbujiro zuio la aina hiyo litafanyika kila mwezi wakati wa mbalamwezi.

“Tunatarajia kufungulia shughuli za uvuvi kuanzia Jumanne (Februari 8). Tunawashukuru wavuvi wa dagaa kwa ushirikiano waliouonyesha kwa kusitisha shughuli kwa siku 15 kuruhusu mazao ya samaki kuongezeka,” alisema Mbujiro.


Akizungumza kwa njia ya simu jana, Katibu Mkuu wa Chama cha Wavuvi Tanzania (Tafu), Jephta Machandalo alisema chama hicho kinaunga mkono utekelezaji wa sheria ya kusitisha shughuli za uvuvi kwa muda maalumu wakati wa mbalamwezi kutoa nafasi kwa dagaa na samaki kuzaliana bila usumbufu.

“Kuna wakati wavuvi wenyewe wanasitisha uvuvi kipindi cha mbalamwezi kutokana na changamoto ya dagaa kuadimika, lakini katika miaka ya hivi karibuni mzunguko wa dagaa ulikuwa mkubwa na unaendelea kwa kipindi chote cha mwezi kabla ya hali kuanza kubadilika katika siku za hivi karibuni kwa dagaa kuadimika wakati wa mbalamwezi,” alisema Machandalo.

Alisema dagaa wanapoanza kuadimika ni lazima uvuvi usitishwe na ama wavuvi wenyewe au mamlaka za Serikali kuepusha hatari ya kuvua watoto na mazalia ya samaki, hasa nyakati za mbalamwezi.

Mvuvi wa dagaa katika Mwalo wa Kayenze, Mandondo Maro alisema uamuzi wa kusitisha uvuvi ulitokana na maombi ya wavuvi wenyewe kwa Serikali kunusuru mazao ya samaki.

Mchuuzi wa dagaa katika Mwalo wa Mswahili, Regina Mumbei alisema licha ya nia njema ya kuongeza mazalia na upatikanaji wa dagaa na aina nyingine ya samaki, zuio la uvuvi kwa siku 15 huwasabishia hali ngumu kiuchumi hasa uamuzi huo unapochukuliwa ghafla bila wadau kutaarifiwa mapema.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments