Wadau: Askari msiwafanye waendesha bodaboda, bajaji chanzo cha mapato

Askari wa usalama barabarani Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa wametakiwa kuacha kuwafanya vijana waendesha bodaboda na bajaji kuwa chanzo cha mapato yao ili waweze kurejesha marejesho ya mikopo yao kama inavyotakiwa.

Hayo yamebainishwa na katibu mwenezi wa CCM wilayani hapa, Dickson Mtevele wakati wa kukabidhi mkopo wa bajaji 10, bodaboda tano pamoja na pikipiki ya kubebea mizogo (guta) moja zilizotolewa na Benki ya NMB tawi la Mafinga kwa ajili ya vijana hao.

Mtevele amesema Jeshi la Polisi kama walivyoweka utaratibu katika maeneo mengine ili kukomesha vitendo vya kihalifu, basi na hilo la maslahi binafsi ya askari likomeshwe ili vijana hao waweze kufanya kazi zao vizuri na kipato anachokipata kiweze kurejesha mkopo wake na siyo kuishia mifukoni mwa watu.

“Vijana hawa wengi wao wanaendesha bajaji na bodaboda, marejesho yao wanayafanya kila siku ndio maana hata leo hapa wengine wameshindwa kuja sio kwa sababu ya uzembe, ni kwa ajili ya tozo zimekuwa nyingi, jambo linalowafanya washindwe kufanya marejesho kwa wakati,” amesema Mtevele.

Katibu huyo amesema Serikali na vyombo vyake wanapaswa kuhakikisha kwamba eneo la usafirishaji linakuwa salama kwa sababu eneo hilo limeajiri vijana wengi kwa ajili ya kujipatia kipato chao.

Pia, amesisitiza benki ya NMB tawi la Mafinga kuendelea na programu hiyo ya kuwakopesha vijana hao kila baada ya miezi mitatu ili kila kijana kwenye umoja huo waweze kumiliki Bajaji na bodaboda zao wenyewe jambo ambalo litawasidia kutoa ajira kwa vijana wenzao.

Kwa upande wake, mkuu wa kitengo cha usalama barabarani wilayani hapa, Hassan Kimaro amesema endapo kila dereva wa bajaji na bodaboda atafuata sheria na taratibu kama inavyotakiwa, hakuna askari atayekuwa na shida naye.

“Niwaombe madereva bajaji na bodaboda kuendelea kuzingatia utaratibu na sheria za usalama barabarani ikiwemo kukata bima kwa ajili ya usalama wa vyombo vyao kwa sababu madhara ambayo yanatokana na ajali za barabarani ni makubwa, hivyo wanapaswa kuzingatia masuala hayo,” amesema Kimaro.

Meneja wa NMB tawi la Mafinga, Focus Lubende amewaasa madereva hao kuwa uaminifu ndio jambo la msingi katika urejeshaji wa mikopo hiyo ili kuweza kutoa fursa ya upataji wa mikopo hiyo kwa madereva wengine.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments