Wanafunzi kidato cha kwanza wasiofika shule kusakwa nyumba kwa nyumba

Halmashauri ya Manispaa ya Lindi  imesema itafanya msako nyumba hadi nyumba na kuwachukulia hatua kali za kisheria wazazi na walezi wa wanafunzi 118 ambao hawajafika shuleni hadi sasa.

Mkuu wa Wilaya Lindi, Shaibu Ndemanga ameyasema hayo wakati alipokuwa anazungumza na Mwananchi Digital kuhusu mkakati  wa uboreshaji elimu  kwenye wilaya hiyo.

Ndemanga amesema wameandaa kikosi kazi ambacho kitapita kila nyumba  kwa lengo lakuwasaka wanafunzi  kidato cha kwanza  wasiofika shuleni hadi sasa na watoro wa kudumu.


Amesema watendaji wa kijiji na kata watashirikishwa kwenye kampeni hiyo ya kawasaka watoto shule za msingi na sekondari na wale wasio fika shuleni mpaka sasa.

Kwa upande wake, Afisa Elimu Sekondari Manispaa ya Lindi,  Rehema Nahale amesema sekta  hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo mwamko mdogo wa wazazi kuhusu masuala ya elimu, upungufu wa walimu 214 wa shule za msingi na 111 shule za sekondari, umbali mrefu kutoka nyumbani  kwenda shuleni na kurudi.

"Sisi kama idara ya elimu tuna jitahidi kutoa elimu kwa wazazi na wanafunzi waone umuhimu wa elimu," amesema Rehama.

Nahale  amesema mwaka wa masomo 2021 na 2022 wanafunzi 1,369 walisajiliwa kufanya mitihani ya upimaji wa majaribio  kwenye shule 23 za sekondari kidato cha nne zilizosajiliwa, lakini wanafunzi 106 walifeli  na wanafunzi 2855 kidato cha pili walifanya mtihani wa upimaji  89 walifeli.

Saidi Magega mzazi amesema wanajua umuhimu wa elimu lakini changamoto  walikuwa nayo ni hali ngumu ya maisha  kwani wanashindwa kupata mahitaji muhimu yanayotakiwa shuleni.

""Sio kama hatutaki kupeleka wanafunzi wakasome ila hali ngumu hakuna hela ya kununua sare," amesema Magega.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments