YANGA SC YAIPIGIA HESABU KALI TP MAZEMBE

Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV
KIKOSI cha Yanga SC kimesafiri kuelekea nchini Tunisia kupitia Dubai kwa ajili ya mchezo wa kwanza wa Michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika (CAF CC) dhidi ya US Monastir ya nchini humo, mchezo utakaopigwa kwenye dimba la Olympic Stadium of Rades (Stade Hammadi Agrebi) jijini Tunis, Februari 12, 2023.

Katika mchezo huo dhidi ya US Monastir ya Tunisia, Yanga SC wameondoka nyumbani nchini Tanzania wakiwa na matumaini makubwa ya kufanya vizuri kwenye mtanange huo wa kwanza wa Kundi D la Michuano hiyo ya pili kwa ukubwa barani Afrika.

Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam kabla ya safari ya kuelekea Tunisia, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga SC, Ally Kamwe amesema wanatambua umuhimu wa alama tatu katika kila mchezo wa Kundi hilo lenye timu za US Monastir ya Tunisia, TP Mazembe ya DR Congo na Real Bamako ya Mali.


"Tunaondoka Dar es Salaam leo saa 9:25 alasiri tukiwa na Wachezaji 25 na Benchi la Ufundi watu sita kuelekea Dubai, ambapo tutapumzika hapo na kesho tutaondoka kuelekea Tunisia,

tunaondoka pamoja na Golikipa Aboutwalib Mshery akienda kwa ajili ya matibabu lakini Kocha Nabi tayari ameshatangulia Tunisia kwa ajili ya maandalizi,” amesema Ally Kamwe.

Hata hivyo, baada ya mchezo huo dhidi ya US Monastir, Wananchi watakuwa na kibarua kizito Februari 19, 2023 kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam dhidi ya miamba ya soka nchini DR Congo, TP Mazembe ikiwa ni mchezo wa pili wa Kundi D la Michuano hiyo ya CAF CC.

"Hii siku ya Jumapili dhidi ya TP Mazembe ni muhimu sana, na tumeipa jina maalum, ‘Wananchi Super Sunday’ maana ndio utakuwa mchezo mkuwa barani Afrika kwa hiyo siku ya Jumapili,” amesema Ally Kamwe.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments