Bunge latunga kanuni ngumu kwa wanahabari, wadau wang’aka

Kanuni hizo ambazo zimechapishwa katika Gazeti la Serikali (GN) ya Machi 21, 2023 zimeeleza maeneo yanayoruhusiwa kupiga picha na kamera zitakazotumika zitalazimika kuruhusiwa na katibu wa Bunge.

Kanuni hizo zimesainiwa na Katibu wa Bunge la Tanzania, Nenelwa Mwihambi, Februari 7, 2023.


Mbali na hayo, waandishi wamepangiwa namna ya kuripoti habari za Bunge ambapo kanuni hizo zinayataja mambo ambayo hayataruhusiwa kuripotiwa ni yale ya faragha.

Kanuni hizo zinasema masuala hayo ni yale ambayo habari zake zikitolewa kwa waandishi wa habari kabla ya wakati wake zinaweza kuathiri uamuzi wa kamati na pia kusababisha ukiukwaji wa kanuni za Bunge.

Masuala hayo ni kazi zote zinazopelekwa kwenye Kamati na Spika ili kupata mapendekezo ya hatua za kuchukuliwa na Bunge na shughuli zote za uchambuzi wa hoja mbalimbali zilizoko mbele ya kamati.

Mengine ni shughuli zote zinazotekelezwa kwa utaratibu wa kiuchunguzi, shughuli zote za kiuchunguzi zenye utaratibu uliowekewa masharti zinazotekelezwa na kamati na shughuli zote zinazotekelezwa na kamati ndogo na kamati zinapofanya ziara za kiuchunguzi.

Kanuni hizo zimetaja kamati zinazotekeleza majukumu kwa faragha ni Kamati ya Uongozi, Kamati ya Kanuni za Bunge, Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC), Kamati ya Hesabu ya Serikali za Mitaa (LAAC) na Kamati ya Bajeti.

Pia, inasema taarifa zenye uwazi wenye mipaka kuwa ni taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) inapowasilishwa bungeni inakuwa wazi kwa vyombo vya habari.

Taarifa nyingine ni mchakato wa kamati hizi kuwahoji maofisa masuuli kuhusiana na taarifa ya CAG utakuwa wazi hadi hatua ambayo Kamati inataka kufanya uamuzi wa kutoa mapendekezo ya hatua za kuchukuliwa na Bunge, ambapo Kamati itafanya kazi zake kwa faragha.

Kanuni hizo zimesema iwapo mchakato wa kuhoji maofisa masuhuli unaofanywa utakuwa ni wa kiuchunguzi, mchakato utafanyika kwa faragha.

Kuhusu upigaji wa picha, kanuni hizo zimesema upigaji wa picha katika ukumbi wa Bunge na maeneo ya Bunge utazingatia heshima, utu na staha.

Pia alisema vifaa vitakavyotumika katika upigaji picha vitaidhinishwa na Katibu kabla ya kupiga picha katika ukumbi wa Bunge na maeneo ya Bunge.

“Mpiga picha atakapokuwa kwenye ukumbi wa Bunge ataelekeza kamera yake kwa Spika au Mbunge anayezungumza wakati huo,”zilisema kanuni hizo.

Pia mpiga picha anaweza kuacha kuelekeza kamera kwa Spika au Mbunge na kuelekeza sehemu nyingine pale ambapo kuna tukio jingine linalohusiana na shughuli inayoendelea.

Aidha, kanuni hizo zimetaja maeneo yasiyoruhusiwa kupiga picha ni maeneo ya ukaguzi wa usalama, benki, mgahawa, zahanati ya Bunge, maegesho ya magari, kumbi zote za kupumzikia wageni na jengo la utawala na mengine yatakayoamuliwa na Katibu.

Hata hivyo, upigaji picha katika maeneo hayo unaweza kuruhusiwa kwa kibali kitakachotolewa na Katibu.
Kanuni hizo zimesema chombo cha habari au mtu atakayekiuka mwongozo huu anaweza kuchukuliwa hatua za onyo na kusimamishwa kwa muda kuchukua na kutoa habari za Bunge.

Pia zimeeleza hatua nyingine ni kufutiwa kibali cha ukusanyaji wa habari na utoaji wa habari za Bunge.


Aidha, kanuni hizo zimesema mtu au chombo cha habari kitakachokiuka masharti ya mwongozo huo kitapata fursa ya kusikilizwa na katibu kabla ya kuchukuliwa hatua.

Kutokana na kanuni hizo, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wakariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile alisema, “tumesikia, tutazichambua, tutawasiliana na uongozi wa Bunge na kwa nini tunataka kurudisha nyuma uhuru wa habari.”

Naye Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari ya Dodoma (CPC), Mussa Yusuph alisema ameshtushwa na hizo kanuni kutokana na kutungwa wakati serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imejipambanua katika kutanua wigo wa masuala ya kidemokrasia na uhuru wa kujieleza.

Amesema Rais Samia aliweza kufungua vyombo vya habari vilivyofungwa, kupunguza ada za usajili katika mitandao ya kijamii lakini wakati huo huo kuna taasisi nyingine zinakuja na mitizamo ambayo inaaminika ni kurejesha nyuma jitihada za Rais Samia.

“Mimi maoni yangu kanuni hizo zirejewe upya na kama kulikuwa na mtizamo uliosababisha kuja kwa hizo kanuni, wanaweza kufungua meza ya majadiliano na upande wetu (waandishi wa habari) tukaja na kanuni ambazo zitakuwa rafiki,” amesema.

Amesema kanuni rafiki zitawezesha kuwapasha vyema wananchi kuhusu kinachoendelea bungeni kwasababu chombo hicho ni mali yao.



TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments