Chadema yaacha kuwahoji kina Mdee mahakamani

Chama cha Demokrasia na Maendeleo kimefunga kuwahoji wabunge  watatu miongoni mwa wengine 19 wa viti maalum waliofukuzwa uanachama na chama hicho, kikisema kuwa hakina maswali zaidi kwa wabunge hao.

Wabunge walioachwa kuhojiwa maswali ya dodoso leo Jumatatu Machi, 6, 2023 ni pamoja na Halima Mdee, Ester Bulaya na Ester Matiko.

Wabunge hao 19 wakiongozwa na aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha), Halima Mdee walifukuzwa uanachama Novemba 2020 baada ya kwenda bungeni Dodoma kuapishwa bila idhini ya chama hicho.


Hata baada ya kukata rufaa kupinga uamuzi wa Kamati Kuu wa Novemba 27, 2020, chama hicho kiliitupa rufaa yao kupitia kikao Baraza kuu la chama hicho Mei 11, 2022 mbele ya, na hatimaye waliamua kufungua kesi Mahakama Kuu.  

Akizungumza leo Machi 6 wakati kesi hiyo iliitwa kwaajili ya Jesca Kishoa kuendelea kuhojiwa maswali ya dodoso, Wakili wa wajibu maombi, Hekima Mwasipu, amesema kesi hiyo ilipaswa kuendelea kwa Mbunge wa Viti Maalumu, Jesca Kishoa lakini kwa upande wao wamefunga.

 “Kesi hii leo imekuja kwaajili ya kuendelea na usikilizwaji na kwa kumhoji mleta maombi wa 12 Jesca Kishoa, tumeamua kufunga hatutakuwa na maswali ya dodoso,” amesema Mwasipu mbele ya Jaji, wa Mahakama Kuu, Cyprian Mkeha.

Wakili Mwasipu ameeleza kuwa baada ya kutafakari kwa kina na kushauriana na bodi ya wadhani ya Chadema, hawatakuwa na maswali ya dodoso tena kwa mleta maombi Halima Mdee, Ester Bulaya na Ester Matiko.

Kwa upande wake Wakili wa waleta maombi Ipilinga Panya ameieleza mahakama kuwa kuwa hawana pingamizi na hoja zilizotolewa na wajibu maombi ya kufunga dodoso.

Kesi hiyo inatarajiwa kuendelea katika hatua ya mahojiano Machi 9 na 10 ambapo mawakili wa waleta maombi, wameomba baadhi ya wajumbe wa bodi ya wadhamini kufika mahakamani kwaajili ya kuhojiwa.


Wabunge hao akiwemo Halima Mdee ambaye alikuwa mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha), na wenzake 18 wamefungua shauri hilo Mahakama Kuu Masjala Kuu, wakipinga kufukuzwa uanachama, kwa utaratibu wa Mapitio ya Mahakama (Judicial Review).

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments