Recent-Post

Chongolo awashangaa Ma-DC kushindwa kutatua migogoro ya wafugaji

Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo amesema kuwa mifugo imekuwa sehemu mojawapo inayosababisha migogoro katika mikoa kati ya 19 hadi 20 nchini lakini akasema ng’ombe hawana mbawa.

Chongolo ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Machi 13, 2023 kwenye mkutano wa mafunzo wa wakuu wa wilaya unaolenga kuwajengea uwezo.

Katibu Mkuu amepewa nafasi ya kusalimia ndipo akasema katika ziara anazopita kwenye mikoa mbalimbali alibaini tatizo hilo huku wakuu wa wilaya ambao wana mamlaka yote wakiwepo kitu kilichomshangaza.


Amesema mifugo haiwezi kuhama kutoka eneo moja kwenda jingine bila kupita ardhini na wanakopita kuna mamlaka zote kuanzia ngazi ya vijiji lakini wanaruhusu na mwisho wake wanakwenda kusababisha migogoro katika baadhi ya maeneo.

“Timizeni wajibu wenu mtakuwa salama,mtalindwa na mamlaka zilizowatea kwani dhamana mliyopewa ni kubwa na CCM inategemea matokeo chanya kutoka kwenu kwa hiyo mkawe suluhisho,” amesema.

Chongolo ambaye amejitambulisha kuwa aliwahi kuwa mwenyekiti wa wakuu wa wilaya Tanzania, ameiomba Serikali kuwakumbuka katika mafungu (OC) kwani mara nyingi wamekuwa wakicheleweshewa hata kufanya mambo mengine kukwama.

Kabla ya kuteuliwa nafasi ya Katibu mkuu wa CCM, Chongolo alitumikia Wilaya za Longido na Kinondoni kwa nafasi ya mkuu wa wilaya hivyo amesema kuwa anayatambua majukumu yote ya cheo hicho.

Ametaja kuwa Mkuu wa wilaya ndiyo mwenyekiti wa kamati nyingi ndani ya eneo lake ikiwemo kuwa na mamlaka kwa mtu yeyote anayeshukiwa kuwa ni mchawi katika eneo hilo kwa hiyo akawaomba wakuu wa wilaya kujiamini.

Post a Comment

0 Comments