DOLA BILIONI 1.9 KUIMARISHA GRIDI YA TAIFA NCHINI

Waziri wa Nishati, January Makamba amesema kuwa Serikali imetenga fedha kiasi cha Dola za Marekani bilioni 1.9 kwa ajili ya miradi ya kuimarisha gridi ya Taifa kwa kipindi cha miaka minne.

Makamba amesema hayo wakati wa uwasilishaji wa taarifa ya utekelezaji wa Bajeti ya Mwaka 2022/2023 kwa wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Jijini Dodoma, Machi 23, 2023.

"Katika Mwaka wa fedha 2022/2023 mradi huu umetengewa sh. Bilioni 500 kwa lengo la kufanya usanifu wa mradi, kupata wakandarasi, kununua vifaa na kuanza utekelezaji wa mradi," amesema Makamba.

Waziri Makamba amefafanua kuwa huu mradi unahusisha ununuzi na ufungaji wa mashine umba 6,000, kusimika nguzo 380,000 za umeme, kununua na kufunga nyaya zenye urefu wa kilomita 46,200 za kusambaza umeme, kununua na kufunga mita za LUKU 700,000.

Amesema fedha hiyo itawezesha kujenga njia za kusafirisha umeme zenye urefu wa kilomita 948 zenye msongo wa kV 132 na kV 22, kujenga vituo 14 vya kupoza umeme wa 220/33 kV na 132/33 kV pamoja na kununua na kufunga mashine umba 66 za ukubwa wa MVA 50, MVA 60, MVA 90 na MVA 120.

"Serikali kupitia mradi huu kwa kushirikiana na Shirika la Umeme nchini (TANESCO) imefanikiwa kuunganisha Mkoa wa Kigoma katika Gridi ya Taifa kupitia kituo cha Nyakanazi pamoja na kuunganisha Wilaya ya Ngara na Biharamulo kupitia kituo hicho hicho cha Nyakanazi," amesema Makamba.

Uthamini wa mali za Wananchi watakaopisha ujenzi wa miradi ya umeme imefanyika kwa mradi wa Tabora - Katavi, Tabora - Kigoma, Shinyanga -Simiyu na uthamini unaendelea kwa miradi ya Benako - Kyaka, Songea - Tunduru - Masasi, Kiyungu - Rombo, Kasiga - Lushoto, Mkata - Kilindi, Pugu - Mkuranga na Bunda - Ukerewe.

“Tathimini ya athari za mazingira imekamilika kwa miradi ya Tabora - Katavi, Tabora - Urambo na Mabibo - Kinyerezi. Kwa miradi ya Benako - Kyaka, Shinyanga – Simiyu na Ilala – Kurasini taarifa ya athari za kimazingira tayari imewasilishwa Baraza la mazingira nchini (NEMC) ili kupata vyeti,” amesema Makamba.

Kwa Miradi iliyobaki ya Songea-Tunduru, Tunduru- Masasi, Kiyungu-Rombo,Kisiga-Lushoto, Mkata- Kilindi,Pugu-Mkuranga,Kibaha-Zegereni na Bunda- Ukerewe tathmini ya athari ya mazingira imeanza kufanyika.

Kamati hiyo ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeishauri wizara kuongeza usimamizi katika utekelezaji wa Miradi ya umeme nchini.

Kikao hicho kimehudhuriwa na Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato, Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Athuman Selemani Mbuttuka, wajumbe wa Bodi kutoka taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Nishati, Wakurungezi kutoka taasisi hizo pamoja na watendaji wengine kutoka Wizara na taasisi.

Waziri wa Nishati, January Makamba akizungumza jambo wakati wa uwasilishaji wa taarifa za utekelezaji wa Bajeti ya Wizara ya Nishati kwa kipindi cha mwaka 2022/2023 kwa wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Machi 23, 2023 jijini Dodoma.


Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dunstan Kitandula akiongoza kikao wakati wizara ya Nishati ilipowasilisha taarifa ya utekelezaji wa Bajeti ya Wizara kwa kipindi cha mwaka 2022/2023.

Wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini pamoja na Watendaji walioshiriki kikao cha kujadili taarifa ya utekelezaji wa Bajeti ya Wizara ya Nishati kwa kipindi cha mwaka 2022/2023.

Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato (wa kwanza kushoto) akiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba (wa kwanza kulia) pamoja na Mkurugenzi wa Shirika la umeme Tanzania, Maharage Chande (Katikati), wakiwa kwenye kikao cha kujadili taarifa ya utekelezaji wa Bajeti ya Wizara ya Nishati kwa kipindi cha mwaka 2022/2023.

Baadhi ya watendaji wa Wizara ya Nishati na watendaji kutoka taasisi zilizopo chini ya Wizara walioshiriki kikao cha kujadili taarifa ya utekelezaji wa Bajeti ya Wizara ya Nishati kwa kipindi cha mwaka 2022/2023


.Na Timotheo Mathayo, Dodoma. 

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments