Idadi ya bia kunywa kwa siku yawa gumzo

Kauli ya watalaamu wa afya kuhusu kiwango cha bia kinachoshauriwa kutumiwa na mtu kwa siku, imezidi kuibua maoni tofauti, safari hii wachambuzi wakijikita katika ujazo wa chupa, wingi wa kileo, afya ya mnywaji na mchanganyiko wa kinywaji chenyewe.

Akizungumza na Mwananchi jana kuhusu hoja ya unywaji wa bia zenye mchanganyiko tofauti, Profesa Harun Nyagori, daktari mshauri mwandamizi wa magonjwa ya ndani na maradhi ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), alisema ni muhimu kutambua tofauti hiyo.

“Ukisema bia mbili bila kusema unaamaanisha bia ya aina gani, haitakuwa na maana. Bia zinatofautiana, zipo aina zaidi ya 40, ndiyo maana unasikia kuna extra lager, lager, logic nakadhalika, hivyo ni lazima uwe specific (utaje upekee),” alisema Profesa Nyagori.

Hoja ya pili inayodhoofisha hoja hizo za unywaji wa bia moja au mbili ni kuhusu tofauti ya kilevi kilichomo kwenye bia husika.

Profesa Nyagori alitolea mfano kuwa kuna bia zina kilevi cha asilimia 4.4, 4.5, 5.0, 5.5 au zaidi hivyo si sahihi kuhitimisha idadi ya unywaji wa bia bila kueleza tofauti hiyo.

Alisema kuna magonjwa mtu anaweza akawa anaugua lakini hata akinywa bia hawezi kudhurika na yapo mengine ambayo tiba yake haimruhusu mgonjwa aguse aina yoyote ya kilevi.

“Kuna wagonjwa tunawaruhusu kunywa ‘red wine’ kwa hiyo tukisema hawaruhusiwi kabisa haileti maana lazima uonyeshe pia upekee” alisema.

Wakati mjadala huo ukiendelea, mwenendo wa uzalishaji wa bia nchini katika vipindi vya miaka minne iliyopita, unaonyesha kushuka kwa lita milioni 33.

Mwaka 2018 uzalishaji ulikuwa lita milioni 413, mwaka 2019 lita milioni 319, mwaka 2020 lita milioni 389, mwaka 2021 lita milioni 380.

Hata hivyo, Profesa Abel Kinyondo kutoka Idara ya Uchumi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), aliliambia Mwananchi kuwa miongoni mwa sababu za kushuka huko sio tu ni mahubiri ya watalaamu wa afya na viongozi wa dini, bali changamoto ya hali za kiuchumi.


“Watu huachana na vitu vya anasa ikiwamo unywaji wa pombe katika kipindi kigumu cha uoatikanaji wa fedha tu,” alisema

Mwanasaikolojia, Charles Muhando alisema licha ya changamoto za kiuchumi, elimu ya madhara itolewayo kwa mifano hai hivi sasa inaendelea kuwafanya watu watambue namna gani ya wanaweza kulinda afya zao.


Mkanganyiko

Mei 2018, gazeti hili liliripoti taarifa ya utafiti wa wanasayansi walioonya unywaji wa glasi moja ya bia au ya divai kwa siku, unaweza kusababishia saratani ya ngozi.

Septemba mwaka jana, Mwenyekiti wa Shirikisho la Magonjwa yasiyo ya Kuambukiza Tanzania, Profesa Andrew Swai alisema mwanaume anatakiwa kunywa chupa mbili za bia kwa siku, ili ajiweke salama dhidi ya magonjwa yasiyo ya kuambukiza huku mwanamke akitakiwa kunywa chupa moja.

Miezi miwili baadaye, gazeti hili likaripoti tena taarifa za matumaini ya wataalamu wa afya waliosema kunywa pombe kwa kiasi si jambo baya au lenye madhara kiafya, lakini kiwango kikizidi husababisha madhara si tu ya kiafya, bali pia kiuchumi na kijamii.

Kwa mujibu wa kitabu cha mtindo wa maisha na magonjwa yasiyoambukiza kilichotolewa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Shirikisho la Vyama vya Magonjwa yasiyoambukiza Tanzania (TANCDA), kuna madhara mengi ya unywaji kupindukia, ikiwemo baadhi ya viungo kushindwa kufanya kazi kikamilifu.

Profesa Mohamed Janabi, Hospitali ya Taifa Muhimbili na Dakatri Bingwa wa masuala ya Moyo anasema kitaalamu inashauriwa mtu atumie kati ya bia moja hadi mbili tu kwa siku na ziwe na mpishano wa saa moja na kwa wale wanaotumia vinywaji vikali wanashauriwa kunywa “shoti” moja tu ili kuulinda moyo.


“Siku hizi kuna magonjwa mengi ambayo yanasababishwa na mtindo wetu wa maisha, ni vema kila mmoja wetu akafahamu hali yake na kubadilisha mfumo wake wa maisha ili ajiepushe na magonjwa yanayoepukika” alisema

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments