Kamati Yaridhishwa Na Utekelezaji Ujenzi Wa Bomba La Mafuta.


Kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa Mradi wa Bomba la Mafuta ghafi la Afrika Mashariki linalojengwa kutoka nchini Uganda hadi Tanga, Tanzania lenye urefu wa kilomita 1,443.

Mwenyekiti wa kamati hiyo ya Bunge, Dunstan Kitandula amekiri kuridhishwa na kasi ya ujenzi wa mradi huo, Machi 16, 2023, wakati wa ziara ya kukagua utekelezaji wa mradi huo wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki kwa upande wa Tanzania.

Kamati hiyo imefika katika kijiji cha Changoleani ili kukagua utekelezaji wa mradi huo wa Bomba la Mafuta Ghafi ambalo nchi za Tanzania na Uganda ni wabia wa mradi.

"Kamati imefika hapa mkoani Tanga katika kijiji cha Changoleani ili kujiridhisha na kasi ya utekelezaji wa ujenzi wa Bomba la Mafuta kwa kuwa Serikali ya Tanzania ni wabia kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na inamiliki asilimia 15 katika mradi wakati wenzetu wa Uganda wanamiliki asilimia 15, na asilimia 70 zilizobaki ni za mwekezaji," amesema Kitandula.

"Kupitia umiliki huu Bunge liliidhinisha fedha ya ujenzi wa mradi, hivyo kamati imefika hapa ili kuona matumizi ya fedha hizo na baada ya kamati kutembelea eneo la mradi imebaini kuwa maandalizi ya ujenzi wa gati yamekamilika na wakandarasi wapo tayari kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo," alieleza Kitandula.

Kitandula ameitaka Serikali iendelee kusimamia na kufuatilia kwa karibu ujenzi wa mradi huo ambao bomba hilo la mafuta ghafi litapita katika Mikoa minane ambayo ni Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Manyara na Tanga ili uweze kukamilika kwa wakati.

Akizungumza na Waandishi wa Habari wakati wa ziara hiyo, Mratibu wa Mradi wa Ujenzi wa Bomba la Mafuta ghafi (EACOP), Asiadi Mrutu amesema kuwa mradi huo umeinua uchumi wa wananchi hasa kwa mikoa yote ambayo mradi huu unatekelezwa kwa kuwa watu zaidi ya 400 wamepata ajira za muda na kudumu, wazawa wakiwa ni 350 na 50 wanatoka nje ya nchi.

Mrutu amesema licha ya upatikanaji wa ajira za kutosha, pia itaimarisha mahusiano baini ya Tanzania na Uganda kwa kuwa mradi huu unatekelezwa na Nchi hizo mbili.

Kuhusu ulipaji wa fidia kwa wanaohama kupisha ujenzi wa bomba hilo, Kamati ilielezwa kuwa fidia kwa wananchi wanaopisha ujenzi huo inaendelea kutolewa bila matatizo na hadi Machi 8, 2023 jumla ya watu 9,276 walikuwa wamesaini mikataba ya fidia.

Kati yao watu 8,479 sawa na asilimia 91.4 wamelipwa fidia na wengine 232 waliobaki wanaendelea kupatiwa elimu na kusainishwa mikataba ya fidia.

Ziara hiyo imehudhiriwa na Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato pamoja na watendaji wengine kutoka Wizara ya Nishati pamoja na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).

Maelezo ya Picha

1. Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dunstan Kitandula (wa tatu kushoto) akiwa na wajumbe wa kamati hiyo walipotembelea Kijiji cha Changoleani, Kata ya Mabanda mkoani Tanga ili kukagua utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki linalojengwa kutoka Tanga hadi nchini Uganda.

2. Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Waziri Kindamba (wa tano kulia) akiwa katika picha pamoja na Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dunstan Kitandula na wajumbe wa kamati hiyo walipofika ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga kwa ajili ya kutembelea Mradi wa Ujenzi wa Bomba la Mafuta.

3. Baadhi ya Miundombinu inayoendelea kuwekezwa kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi mkoani Tanga katika Kijiji cha Changoleani.

4. Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini wakiwa pamoja na watendaji mbalimbali kutoka Wizara ya Nishati na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) katika Kijiji cha Changoleani mkoani Tanga, mahali lilipo jiwe la Msingi wa Mradi huo.






 Na Timotheo Mathayo, Tanga.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments