Kishindo cha maridhiano

Ni kishindo cha maridhiano, ndivyo unavyoweza kusema baada ya Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha) kumwalika Rais Samia Suluhu Hassan naye akakubali kuwa mgeni rasmi katika mkutano wa Siku ya Wanawake Duniani utakaofanyika mkoani Kilimanjaro.

Mkutano huo utakaofanyika Machi 8, mwaka huu, utakuwa ni tukio la kihistoria na la kwanza nchini, kwa chama cha upinzani kumwalika mkuu wa nchi na yeye akakubali kushiriki shughuli yake tangu kuanza kwa mfumo wa siasa za vyama vingi nchini mwaka 1992.

Msimamo huo ni mwendelezo wa hatua kadhaa za maridhiano zilizopigwa, tangu viongozi wa CCM, Chadema na Serikali waanze vikao vya kufanikisha suala hilo.


Vuguvugu la maridhiano baina ya vyama hivyo, lilianza Machi 4, mwaka jana baada ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kukubali mwaliko wa Rais Samia Ikulu saa chache mara tu baada ya kutoka gerezani alikokuwa amekaa kwa miezi minane.

Tangu kipindi hicho, wawili hao kupitia vyama vyao na Serikali wamekuwa wakikaa vikao vya pamoja kujadili mambo mbalimbali kuhusu uendeshaji wa siasa nchini.

Pamoja na mambo mengine, masuala kadhaa yametajwa kama matokeo ya maridhiano hayo, ikiwemo kufutwa kwa mashauri mbalimbali yanayohusiana na siasa, mikutano ya vyama vya siasa iliyozuiwa miaka saba iliyopita imeruhusiwa nchini na vikao vya majadiliano kuhusu masuala mbalimbali vinaendelea.


Samia mgeni rasmi

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha jana, Mbowe alisema kwa kuwa siku ya wanawake inaihusu jinsi hiyo kote ulimwenguni, hivyo bila kujali itikadi zao watu mbalimbali mashuhuri wamealikwa.

“Nikitambua namna ambavyo tumefanya kazi na Rais Samia, tumekubali tumualike, naye amekubali kuhudhuria aje awasikie akinamama wa Chadema, kina mama wa upinzani.

“Siku zote anawasikiliza wakina mama wa chama chake, aje awaone atambue kazi kubwa inayofanywa na akina mama wa Chadema kwa hiyo Rais atakuwa mgeni rasmi katika tukio letu na mimi nitakuwepo kumpokea,” alisema.


Alipoulizwa kuhusu mwaliko wa Rais Samia na iwapo amekubali kushiriki, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Zuhura Yunus alisema jambo hilo ni sahihi.

Akifafanua maelezo yake Mbowe, alisema Chadema imefurahishwa na hatua ya mkuu huyo wa nchi kuridhia kusikiliza changamoto za wanawake wa chama hicho, akisisitiza kuwa ni wajibu wake.

Akizungumza kuhusu mkutano wa siku ya wanawake duniani, Katibu Mkuu wa Bawacha, Catherine Ruge alisema maadhimisho hayo yatafanyika Moshi mkoani Kilimanjaro.

Machi 7, mwaka huu alisema wanatarajia kutembelea vivutio mbalimbali na kupanda Mlima wa Kilimanjaro.

“Tayari wanawake 2,613 hadi jana (juzi) wamejiandikisha kushiriki kilele cha siku ya wanawake duniani hii ni kwa Mkoa wa Kilimanjaro pekee, tunawasihi wengine kuendelea kujisajili,” alisema.

Pamoja na hayo, Mbowe alisema kulikuwa na tofauti kubwa kati ya chama hicho na CCM, lakini kwa sasa baada ya maridhiano kumekuwa na nafuu licha ya uwepo wa changamoto mbalimbali.

Hata hivyo, Mbowe alisisitiza kuwa hatua ya chama hicho kuingia kwenye maridhiano haimaanishi wamekoma kuikosoa Serikali na kueleza sera mbadala.

“Tutaendelea na kazi yetu ya upinzani kwa nguvu zote na hatutaogopa kuikosoa Serikali, hatutaona haya kueleza sera mbadala na sisi kazi yetu ya kuiondoa CCM madarakani iko pale pale,” alisisitiza.

Katika hatua nyingine, mwenyekiti huyo alisema juzi walikutana na Rais Samia katika Ikulu ndogo jijini Arusha kuzungumzia maridhiano na wamekubaliana kwamba kazi hiyo itaendelea kufanyika.

“Tumekubaliana na Rais kwamba tuendelee na maridhiano na nimemtaka mambo haya yasiende kama konokono, yaende kwa kasi ili kuhakikisha uchafuzi (uharibifu wa uchaguzi) hautajitokeza tena,” alisema.


Alipoulizwa kuhusu tume ya mabadiliko ya haki jinai, Mbowe alisema bado haijamfikia kwa mapendekezo, lakini chama hicho kipo tayari kutoa ushirikiano katika jambo lolote linaloleta mabadiliko ya sheria na Katiba.

Alieleza katika vikao na CCM na Rais Samia suala hilo walilieleza kwa kina kwa kuwa karibu wote walioshiriki wamewahi kupita magerezani.

Alipoulizwa kuhusu madai ya kupokea ruzuku, Mwenyekiti huyo alisema mtendaji mkuu wa Chadema (John Mnyika) atatoa taarifa hiyo wakati muafaka.

“Sisi chama chetu ni kikubwa sana kina uwezo wa kutoa taarifa zake chenyewe kwa wakati unaostahili, kwa hiyo watendaji wakuu wa chama watajibu hilo wakati muafaka,” alisema.

Ufafanuzi huo ulikuwa unalenga taarifa zilizosambaa mitandaoni jana kuwa chama hicho kimekwishapokea zaidi ya Sh800 milioni za ruzuku ambazo awali kilizikataa kwa madai kuwa ni zao la Uchaguzi Mkuu wa 2020 ulioharibiwa na mamkala.

Hata wabunge wa viti maalumu walioteuliwa baada ya uchaguzi huo hicho, chama kiliwakataa na kesi dhidi ya uamuzi huo inaendelea..

Vilevile, Mbowe alisema chama hicho kinatarajia kuzindua operesheni maalumu itakayoanzia Kigoma, Katavi, Kagera ambako wanatarajia kukutana na Tundu Lissu, makamu mwenyekiti wa Chadema baada ya kutoka safari Ulaya.

Akifafanua kuhusu Lissu, Mbowe alisema mwanasiasa huyo alikwisharudi nchini na sasa amesafiri kwa shughuli maalumu lakini atarudi kuungana na viongozi wenzake kwenye shughuli za chama kuanzia Kanda ya Magharibi.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments