Mbunge alia mgogoro kati ya vijiji tisa na Hifadhi ya Tarangire

Mbunge wa Babati Vijijini (CCM), Daniel Sillo amebainisha changamoto ya kuwepo kwa mgogoro kati ya Hifadhi ya Taifa ya Tarangire na wananchi wa vijiji tisa vinavyopakana na hifadhi hiyo.

Amesema wanyamapori wamekuwa wakivamia mashamba ya wakulima na kuharibu mazao yao lakini kila wakifuatilia kulipwa fidia, wamekuwa wakichelewa kulipwa stahiki zao kwa zaidi ya miaka miwili au zaidi na kile wanacholipwa ni kidogo.

Sillo amebainisha hayo leo Machi 7, 2023 wakati wa ziara ya Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo katika Wilaya ya Babati mkoani Manyara ambako anakagua utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020.


"Hapa kuna mgogoro kati ya vijiji tisa na Hifadhi ya Taifa ya Tarangire. Kuna wakati wanyamapori wanavamia mashamba ya wananchi na kuharibu mazao yao.

"Fidia wanayolipwa ni ndogo na inachukua muda mrefu. Hili linawasababishia wananchi umasikini, tunaomba useme neno katika hili ili wananchi hawa wapate haki zao," amesema Sillo akimweleza Katibu Mkuu Chongolo.

Mbunge huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, amesema kuna shamba la ekari 1,700 ambalo lina mwekezaji lakini hajaliendeleza na halitumiki kwa shughuli yoyote, ameomba shamba hilo wapewe wananchi kwa ajili ya shughuli za kilimo.

"Ndugu Katibu Mkuu, tunaomba shamba hili wapewe wananchi ili wafanye shughuli yao ya kilimo," amesema Sillo huku akishangiliwa na wananchi wa Kijiji cha Magala.

Akizungumzia mgogoro huo, Chongolo amemtaka Waziri wa Maliasili na Utalii, Mohamed Mchengerwa au timu yake iende kuangalia uhalisia wa mambo katika mgogoro huo na kuona namna ya kuutatua.

"Ninakwenda kuzungumza na Waziri wa Maliasili na Utalii. Nitamwelekeza aje hapa au atume wataalamu wake, waje waangalie hali halisi. Nataka waje wawaambie kama mna haki au hamna haki, na kwanini hamna hamna haki ili mjue," amesema Chongolo.


Amesisitiza kwamba atamwelekeza waziri huyo kwenda kushughulikia mgogoro huo sambamba na kuwalipa fidia wananchi walioharibiwa mazao yao kwa hali kulingana na kiwango cha uharibifu uliofanyika.

"Kama mwananchi amelima ekari moja na ikaharibiwa na tembo, basi alipwe fidia halisi inayoendana na ekari moja, siyo wajipangie wao, tathmini ya uzalishaji wa ekari moja ifanyike na mwananchi alipwe haki yake," amesema Chongolo.

Ametoa wito pia kwa wananchi kuacha kuingilia hifadhi kulisha mifugo yao kwa sababu kwa kufanya hivyo wanaharibu mfumo wa ikolojia ndani ya hifadhi, jambo linalosababisha wanyama nao watoke kwenye hifadhi kuja kijijini.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments