Mjadala kuhusu ajira za bodaboda moto

Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema ameendeleza kauli yake kuhusu ajira ya bodaboda, akisisitiza ni laana na chanzo cha umasikini kwa vijana.

Lema ameeleza hayo wakati Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM (Uvccm), Kenani Kihongosi akieleza kukerwa na kauli hiyo akisema inakasirisha kusikia mwanasiasa aliyewahi kuwa kiongozi na kulipwa mshahara na Serikali anawatusi bodaboda.

“Wewe ukipata neema Mungu amekupa uwezo, usidharau wasio na uwezo ukaona hawataki kufanikiwa, umeenda Ulaya umeishi karibu miaka miwili huko... umekuja umetua leo unasema bodaboda ni shughuli ya laana sijui wanakimbiza upepo,” alisema Kihongosi.


Kihongosi alikuwa anazungumzia kauli aliyoitoa Lema kwenye mkutano wa wakeanza wa hadhaa aliofanya jijini Arusha mara tu baada ya kurejea nchini Machi mosi mwaka huu.

Si hilo tu, Lema pia alizungumzia suala la michezo ya kubahatisha iliyowateka vijana na vikoba kwa kina mama kuwa masuala hayo ni sawa na kurasimisha umaskini.

Aweka msisitizo

Akizungumza katika mkutano wa hadhara na wanachi wa Karatu jana, Lema alisisitiza msimamo huo akisema bodaboda si kazi bali ni laana.

Hoja yake hiyo ilitokana na kile alichokifafanua kuwa shughuli hiyo inaongoza kwa kuangamiza uhai wa vijana nchini lakini haiwafaidishi.

“Hakuna kazi imeangamiza vijana kama kazi ya bodaboda, halafu mnasema tusiseme ukweli eti kwa sababu mna kura, mimi siishi kwa ubunge, nataka nitetee watu,” alisema Lema.

Alisema shughuli hiyo na ile ya vicoba kwa wanawake ni mifumo inayorasimisha umasikini kwa Watanzania.

Badala ya kulalamikia kauli hiyo, aliitaka Serikali itafute mbinu ya kuwaondoa wananchi wake kwenye ajira ya “kukimbiza upepo” kwa kutafuta wawekezaji watakaowaajiri kwenye shughuli ambazo hata watakapostaafu watapata ujira.


“Hiyo si kazi ya maana na inazidisha umasikini na umasikini ni laana, kama noma na iwe noma men. Kuna vitu vinaitwa vicoba vinawafanya wanawake kuwa masikini,” alisema Lema.

Kwa mujibu Lema, taasisi za fedha zilipaswa kuwa chanzo cha mitaji kwa wananchi kupitia mawazo yao, huku Serikali ikiwadhamini.

Mwanasiasa huyo aligusia pia changamoto ya elimu inayotolewa nchini, akisema haiakisi uhalisia wa maisha anayokutana nayo mwananchi uraiani.

“Shule unakwenda kujifunza panzi ana miguu mingi, kipepeo ana rangi mbalimbali ukija mtaani hivi havikusaidii kitu, ndiyo maana mimi sitaki kupeleka mwanangu kwenye shule za kata, watasema Lema si mzalendo, uzalendo ni kutokusoma vizuri?” alihoji.

Katika hatua nyingine, mwanasiasa huyo alikiri kumwomba Rais Samia kuwa anataka kurejea nchini na alimkubalia na kumfutia kesi zilizokuwa zinamkabili.

Lakini, alisema ameupata msaada huo kwa kuwa ni kiongozi wa kisiasa mwenye uwezo wa kumfikia Rais.

Ila alisema wapo watu waliodhulumiwa na hawana uwezo kama alionao yeye wa kumfikia Rais, hivyo Katiba mpya ndiyo tumaini lao.

“Kweli nilimwambia mama nataka kuja Tanzania, walinifungulia kesi kweli akanifutia, namshukuru. Lakini nataka afikirie jambo moja, mimi ni kiongozi wa kisiasa nimepata fursa ya kupigania haki yangu, lakini watu wengine hawana uwezo wa kukufikia wewe (Raisa Samia), Katiba mpya ndiyo suluhisho lao,” alisema Lema.

Hata hivyo, Lema alimhakikishia mkuu huyo wa nchi kufanya siasa za kistaarabu akisema hawatamtusi bali watamwambia ukweli.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho, Peter Msigwa alisema bei za bidhaa mbalimbali zinazoendelea kupanda ikiwamo ya maji, zinalenga kumuongezea ugumu wa maisha mwananchi wa kijijini.


TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments