Mtoto wa Rais wa Uganda, Yoweri Kaguta Museveni, Jenerali Muhoozi Kainerugaba ametia nia ya kuwania urais wa nchi hiyo mwaka 2026, kuchukua nafasi ya Baba yake ambaye kwa sasa yupo madarakani kwa takribani miaka 37 ya utawala.
Mapema siku ya Jumatano, kupitia ukurasa wake rasmi wa ‘Twitter’ licha ya kufuta haraka ujumbe huo, Jenerali Kainerugaba alisema atasimama kuwania urais wa nchi hiyo mwaka 2026, “Umetaka niseme milele! sawa, kwa jina la Yesu Kristo Mungu wangu, kwa jina la vijana wote wa Uganda na dunia na kwa jina la mapinduzi yetu makubwa, nitagombea Urais 2026.”
Pia, Mshauri huyo wa Rais, Jenerali Muhoozi Kainerugaba kupitia ukurasa wake huo wa ‘Twitter’, amesema: “Waziri Mkuu wa Uingereza ana umri wa miaka 42, Waziri Mkuu wa Finland ana miaka 37. Baadhi yetu wana umri wa miaka 50. Tumechoka kusubiri milele.”
Awali, Jenerali Muhoozi Kainerugaba alikuwa Kamanda wa Jeshi la Ardhi la nchi hiyo lakini alitolewa katika nafasi hiyo kutokana na tishio lake la kutaka kuivamia nchi jirani ya Kenya, licha ya baadae kusema kuwa alikuwa anatania, huku akiacha mitazamo tofauti baina ya nchi hizo mbili katika masuala ya kidiplomasia.
Hata hivyo, Museveni hajasema chochote kuhusu kuwania Urais wa nchi hiyo mwaka 2026, licha ya Wafuasi wake kumhimiza kuendelea tena katika kipindi kingine cha saba katika utawala wa nchi hiyo ya Uganda tangu mwaka 1986.
JENERALI MUHOZI KAINERUGABA NI NANI?
Ni mtoto wa Rais wa sasa wa Uganda, Yoweri Museveni, Jenerali Kainerugaba alizaliwa nchini Tanzania mnamo Aprili 24, 1974. Alikuwa Kamanda wa Kamandi ya Kikosi Maalum (SFC) mwaka 2008 hadi 2017. Alirudi tena kwenye nafasi hiyo Desemba 2020 hadi 2021.
Jenerali Kainerugaba aliwahi kuwa Kamanda wa Kikosi cha nchi Kavu katika Jeshi la Wananchi wa Uganda (UPDF) kuanzia Juni 24, 2021 hadi Oktoba 4, 2022 na alitolewa kwenye nafasi hiyo kufutia ujumbe wake wa kutaka kuvamia mji wa Nairobi nchini Kenya. SFC na UPDF walimshutumu kwa kutumia madaraka yake vibaya.
Jenerali Kainerugaba na Maafisa wengine wa ngazi za juu walitajwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita (ICC). 2017 Jenerali huyo alichaguliwa kuwa Mshauri wa Rais wa Uganda.
Mnamo, Novemba 30, 2021, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo waliazimia kuweka ulinzi wa kijeshi Mashariki mwa Congo kupitia Oparesheni Shujaa ambayo iliongozwa na Jenerali Muhoozi ikiwa na lengo la kupambana dhidi ya Kundi la ‘Allied Democratic Forces’ (ADF) la nchini Uganda.
Chanzo: Mtandao
0 Comments