RUZUKU KUTOKA REA MKOMBOZI UKAMILISHAJI MRADI WA UMEME LUPALI

Watawa wa Kanisa Katoliki wa Shirika la Wabenediktini, Imiliwaha Njombe, wametoa shukrani kwa Wakala wa Nishati Vijijini kwa kutoa ruzuku inayotumika kukamilisha utekelezaji wa mradi wa umeme wa maji – Lupali utakaozalisha kilowati 317 pindi ukikamilika.


Walitoa shukrani hizo wakati wa ziara ya Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Janet Mbene, Machi 16, 2023 iliyolenga kujionea maendeleo ya utekelezaji wa Mradi huo unaosimamiwa na Watawa hao kwa ufadhili wa REA na wadau wengine.

Akiwasilisha taarifa fupi ya utekelezaji wa Mradi mbele ya Mwenyekiti wa Bodi na Ujumbe aliofuatana nao, Mratibu wa Mradi, Sista Imakulata Mlowe ameeleza kuwa tangu kuanza kwa mradi mwaka 2011, REA imechangia kwa kiasi kikubwa katika hatua zote.

Akifafanua zaidi, Sista Imakulata amezitaja hatua za Mradi ambazo REA imechangia kuwa ni pamoja na gharama za utafiti wa awali, ujenzi wa njia kuu za kusafirishia umeme (kilomita 23.48) na njia ndogo za kusambazia umeme kwa watumiaji (kilomita 30.61

Ametaja nyingine kuwa ni ruzuku iliyotolewa kukamilisha mradi ikihusisha ujenzi wa sehemu ya kupokelea maji, nyumba ya mtambo, uwekaji wa mabomba pamoja na shughuli nyingine za Mradi.

“Tunatoa shukrani za dhati kwa REA na Serikali kwa ujumla kwa kutoa ruzuku ya kukamilishia ujenzi wa mradi. Kupitia ruzuku hii, ndoto ya shirika la Watawa Wabenediktini wa Mtakatifu Getrud, waliopo Imiliwaha, ya kukamilisha ujenzi wa mradi huu, itatimia.”

Akieleza zaidi kuhusu ruzuku iliyotolewa na REA kukamilisha mradi, Sista Imakulata amesema mkataba wake ulisainiwa Desemba 2021 ukiwa na jumla ya shilingi 2,211,507,500 na utekelezaji ulianza Juni, 2022.

Aidha, ameeleza kuwa yapo mahitaji ya kugharamia uunganishaji wa umeme utakaozalishwa kwenda kwenye Gridi ya Taifa hivyo baada ya kupata maelekezo ya kitaalamu kutoka TANESCO na mahitaji ya vifaa vinavyotakiwa, watawasilisha rasmi maombi kwa REA ya kufadhili gharama hizo za uunganishaji ili kuwezesha mradi kufikia utimilifu wake.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini aliwapongeza watawa hao kwa kazi nzuri ya kuanzisha na kusimamia utekelezaji wa mradi huo ambao alisema ukikamilika utaendelea kusaidia jitihada za Serikali za usambazaji umeme vijijini kwa kasi.

Alisema, REA itaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali pamoja na watu binafsi wenye malengo ya kutekeleza miradi ya nishati vijijini ili kuwezesha kutimia kwa azma ya Serikali ya kuwaletea wananchi wake maendeleo.




Ujenzi wa nyumba ya mtambo (power house) ukiendelea katika mradi wa kuzalisha umeme wa maji ya Mto Lupali, Njombe. Mradi huo unatekelezwa na Watawa wa Kanisa Katoliki wa Shirika la Wabenediktini, Imiliwaha kwa ufadhili kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA) pamoja na wadau wengine. Taswira hii ilichukuliwa Machi 16, 2023 wakati wa ziara ya Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Janet Mbene.



Sehemu ya maporomoko ya maji ya Mto Lupali ambayo yatatumika kuzalisha umeme wa kilowati 317 kupitia mradi unaoendelea kutekelezwa na Watawa wa Kanisa Katoliki wa Shirika la Wabenediktini, Imiliwaha Njombe kwa ufadhili wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) pamoja na wadau wengine. Taswira hii ilichukuliwa Machi 16, 2023 wakati wa ziara ya Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Janet Mbene.



Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Janet Mbene (wa pili-kushoto), akizungumza jambo, wakati wa ziara yake iliyofanyika Machi 16, 2023 kukagua maendeleo ya Mradi wa umeme wa maji – Lupali unaoendelea kutekelezwa na Watawa wa Kanisa Katoliki wa Shirika la Wabenediktini, Imiliwaha Njombe kwa ufadhili wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) pamoja na wadau wengine.
Veronica Simba - REA

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments