Recent-Post

Serikali yaja na mwarobaini udhalilishaji wanawake mitandaoni

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali ipo mbioni kubadili sheria za mtandao, ikiwa ni pamoja na kuboresha Kitengo cha SyberCrime (Uhalifu wa Kimtandao) kwani udhalilishaji ni miongoni mwa changamoto zinazokwenda kukomeshwa.

Majaliwa ameyasema hayo leo Ijumaa, Machi 10, 2023 wakati akifungua mkutano wa tano wa uongozi, ulioambatana na mahafali ya nane ya Programu ya Mwanamke Kiongozi yaliyoandaliwa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE).

Amesema usalama wa kimtandao limeendelea kuwa tishio na ni tatizo kubwa, hivyo Serikali imeendelea kuimarisha usalama kwa kuwajengea uwezo wataalamu eneo hilo na kujenga mazingira wezeshi katika sheria na mifumo ya mtandao.


“Katika hili kitengo chetu cha uhalifu wa kimtandao kinafanya kazi kubwa, kuhakikisha kesi zinazotokana na uhalifu wa kidijitali zinashughulikiwa na kupatiwa ufumbuzi haraka,” amesema.

Amesema Serikali itahakikisha inabadili sheria ili kwenda sambamba na mabadiliko ya sayansi na teknolojia kwani inatambua uwepo wa vikwazo mbalimbali hasa katika kumudu gharama za bando na vifaa vya kushiriki mifumo ya kidigitali ambayo inasaidia kuongeza ukuaji wa uchumi.

Waziri Mkuu amesema suala la mabadiliko ya kidigitali ni moja ya vipaumbele vya Taifa kwani maendeleo ya uchumi yanategemea utandawazi.

"Lakini pia katika mabadiliko haya ni muhimu kutambua mchango wa wanawake katika uchumi wetu na kutatua changamoto zinazowakabili wanawake ili waweze kushiriki kikamilifu katika masuala ya uchumi wa kidijitali,” amesema.

Amesema Serikali kwa kutambua umuhimu wa uchumi wa kidijitali, imeendelea kubuni mikakati mbalimbali ambayo itaiwezesha nchi kutumia vema fursa za kiteknolojia zilizopo katika kuinua uchumi.

"Ili kutimiza azma hiyo, tayari Mkakati wa Taifa wa Brodibandi wa mwaka 2021–2025 ambao utawezesha asilimia 80 ya Watanzania kupata huduma za intaneti yenye kasi ifikapo mwaka 2025 umeshaandaliwa.


“Serikali inaendelea na maandalizi ya Mkakati wa Taifa wa Uchumi wa Kidigitali ili kuhakikisha nchi yetu haibaki nyuma katika ulimwengu wa kidijitali," amesema.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Dk Saada Mkuya Salim amewataka ATE kuhakikisha inafikisha Programu ya Mwanamke Kiongozi kwa wanafunzi wa kike walio katika shule za sekondari na vyuo vikuu.

“Mimi ni mnufaika wa hii kozi kule niliipata nikiwa Baraza la wawakilishi lakini tunahitaji kupata mafunzo kutokana na mabadiliko ya teknolojia, kikubwa sasa mafunzo haya yaende ngazi za shule za sekondari na vyuo vikuu ili tupate viongozi wengi zaidi wanawake katika taifa hili tuwapike wangali wadogo,” amesema Waziri Mkuya.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima amesema, “Mambo mengi yamefanyika kiwainua wanawake ikiwemo masuala ya teknolojia, Serikali inapambana kuhakikisha wanawake wanaongezeka katika nafasi za uongozi.”

Mkutano huo uliambatana na mahafali ya nane ya Programu ya Mwanamke Kiongozi, jumla ya wahitimu 65 walitunukiwa vyeti. Washiriki 11 wa programu hiyo walijidhamini wenyewe na wengine 54 wanatoka kwenye kampuni 29.

Post a Comment

0 Comments