Serikali yasitisha huduma za bweni kwa watoto wadogo

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imezitaka shule zote zinazotoa huduma ya bweni kwa madarasa ya kwanza hadi la tano kusitisha huduma hiyo ifikapo mwisho wa muhula wa kwanza mwaka 2023.

Waraka huo ulitolewa na Kamishna wa Elimu wa wizara hiyo, Dk Lyabwene Mtahabwa kwa wadau wa elimu nchini unasema utekelezaji wa waraka huo unatakiwa kuanza Machi Mosi mwaka huu.

Amesema hairuhusiwi kutoa huduma ya bweni kwa wanafunzi wa elimu ya awali na darasa la kwanza isipokuwa kwa kibali maalum kitakachotolewa na Kamishna wa Elimu baada ya kupokea maombi kutoka mdau husika.


Dk Mtahabwa amesema hatua hiyo ni utekelezaji wa mwongozo wa uanzishaji wa usajili wa shule uliotolewa na wizara Novemba 2020.

Amesema kwa upande mwingine malezi na makuzi ya mtoto yanategemea sana mchango mkubwa unaotolewa na familia kupitia wazazi/walezi wa watoto hao.

“Hata hivyo imebainika kuwa kuna baadhi ya shule zimekuwa zikipokea watotro wenye umri mdogo kuanzia darasa la awali hadi darasa la nne,”amesema.

Amesema huduma za bweni kwa wanafunzi wenye umri mdogo ikiwemo wale wa elimu ya awali na darasa la kwanza hadi la nne huwanyima watoto fursa ya kushikamana na familia na jamii zao, kujenga maadili na kushiriki katika shughuli mbalimbali za maendeleo ya familia na jamii zao.

Kwa upande wa makambi, Dk Mtahabwa amesema hairuhusiwi kwa shule yoyote ile kuwa na makambi ya kitaaluma.

Amesema hatua hiyo ni utekelezaji wa Waraka wa Elimu namba 3 wa mwaka 2007 kuhusu kukataza kambi za masomo katika shule za msingi.

“Hata hivyo imethihirika kuwa makambi mengi yamebainika kuwa na mazingira hatarishi kimaadili, usalama na afya za wanafunzi kutokana na kuanzishwa bila kufuata taratibu rasmi za uanzishwaji wa bweni au makazi ya pamoja ya wanafunzi,”amesema.


TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments