SIMBA SC YAFUKUZISHA KOCHA VIPERS SC

BAADA ya kufungwa na Simba SC ya Tanzania, bao 1-0 katika michezo miwili mfululizo ya Michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika, Klabu ya Vipers imevunja mkataba baina yao na Kocha Mkuu raia wa Brazil, Roberto Luiz Bianchi Pellise.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Klabu hiyo ya nchini Uganda imeeleza kuwa mkataba baina yao na Kocha huyo umevunjwa mara moja, huku wakimshukuru Bianchi kwa jitihada zake katika muda wote alipokuwa na Kikosi hicho tangu kupewa mkataba, Januari 10, 2023.

Kocha Bianchi alipewa majukumu ya kukinoa Kikosi hicho cha Vipers SC kwa mkataba wa miaka miwili baada ya Januari 3, 2023 timu hiyo kutangaza kuachana na Kocha wao Mkuu, Roberto Oliveira (Robertinho) ambaye alitimkia katika Kikosi cha Simba SC.

Kibarua cha Kocha Bianchi kilianza Januari 31, mwaka huu dhidi ya Bujumbura United SC katika mashindano ya Stanbic Uganda Cup, mchezo wa kuwania kufuzu hatua ya 32 Bora ya mashindano hayo, mchezo huo ulipigwa kwenye dimba la Kibanjwa P/S Ground.

Viper SC walifanikiwa kufuzu hatua ya 32 Bora ya mashindano hayo baada ya ushindi wa mikwaju ya Penalti 4-1 dhidi ya timu hiyo (Bunjumbura United) ikiwa ni baada ya sare ya 0-0 katika dakika zote 90’ za mchezo huo.

Februari 11, 2023 katika mjini wa Casablanca nchini Morocco, kwenye dimba la Mohammed V, Kocha Bianchi alikutana na dhahama la kufungwa mabao 5-0 na Raja Casablanca kwenye Michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika hatua ya makundi, ikiwa ni mchezo wa Kundi C la Michuano hiyo.

Februari 15, 2023 kibarua kingine cha Kocha Bianchi kilikuwa dhidi ya Jinja North United FC kwenye mashindano ya Stanbic Uganda Cup katika hatua ya 32 Bora ya mashindano hayo na Vipers SC walifanikiwa kufuzu hatua ya 16 Bora kwa jumla ya mikwaju ya Penalti 7-6 baada ya sare ya 0-0 kwenye dakika 90’ za mchezo huo.

Vipers SC walirejea tena kibaruani Februari 18, 2023 kwenye Michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kumenyana na wageni Horoya AC kutoka Guinea kwenye dimba la St. Mary’s Kitende, Entebbe na kulazimishwa sare ya 0-0 katika dakika 90’ za mtanange huo wa pili wa Michuano hiyo.

Kwenye Ligi ya nyumbani, (Uganda Premier League) ilikuwa Februari 21, 2023 Vipers SC wakiwa nyumbani St. Mary’s walilazimishwa sare ya 0-0 na Wakiso Giants FC.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments