TV3 YAINGIA MAKUBALIANO NA BODI YA LIGI KUU

BODI ya Ligi Kuu Tanzania kwa kushirikiana na Tv3 chini ya Startimes Media zimeingia makubaliano ya kurusha ligi ya Championship michezo iliyobaki kwa lengo la kutangaza michezo hiyo na kuipa thamani.


Akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 24, 2023 jijini Dar es Salaam Afisa Habari wa bodi hiyo Karim Boimanda amesema makubaliano hayo ya kurusha matangazo ya Ligi hiyo itaenda kuleta thamani na kutoa fursa kwa wadhamini wengine kuiunga mkono msimu ujao.

"Ligi ya Championship chini imekuwa ni miongoni mwa ligi zenye mvuto katika ukanda wa Afrika Mashariki kwasababu ina wachezaji wengi wa ndani na nje ya nchi ambao wanaleta ushindi kama ilivyo Ligi Kuu isipokuwa changamoto iliyopo hawakuwa na wadhamini pamoja na mtangazo kuruka Mubashara japo tulitoa vibali kwa timu kurusha matangazo kwenye Online Media zao.

Hata hivyo amewapongeza Tv3 kwa kuitika wito wa kudhamini ligi hiyo kwani bodi ya Iigi ilikuwa na kiu kubwa ya kuona wadau hususani televisheni kubwa zinachukua ligi hiyo kuirusha Mubashara.

Mkurugenzi Mwendeshaji wa Tv3 Ramadhan Msemo ameeleza kuwa fursa hii ya kuonesha ligi itawasaidia wachezaji na timu kujitangaza na kujiuza na hivyo kuongeza mapato ya Klabu au wachezaji kununuliwa na Klabu nyingine na kuongeza kipato chao.

Aidha,ameongeza kuwa kuanzishwa kwa TV3 ilikua na lengo la Kuonyesha maudhui ya Kimichezo na kuhakikisha Vijana wanapata fursa ya kutazama mashindano mbalimbali ya kimichezo.

"Tumetoka kuonesha ligi daraja la Kwanza Zanzibar na michezo mingine mbalimbali lengo letu ni kuunga mkono juhudi za kukuza michezo nchini kwa kuhakikisha Tv3 inakuwa sehemu ya kurusha mubashara maudhui ya Michezo nje na ndani ya nchi."

"Tunawashukuru Bodi ya ligi na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa ushirikiano, tumejiandaa kuzionesha mechi zote kwa ubora wa hali ya juu kuanzia Jumamosi hii, tunaamini itakuwa chachu kwa wadau wengine kujitokeza na kuunga mkono,"alisema.

Mkurugenzi wa Masoko wa Startimes David Malisa aliwashukuru TFF kwa kuwapa fursa hiyo akisema kwao wanachukulia kama sherehe akiamini kutokana na idadi ya watumiaji wa kisimbuzi chao watawafikia watu wengi ndani na nje ya nchi.

"Hii ni moja ya ligi kubwa sana, kutakuwa na maudhui mbalimbali kabla na baada ya michezo , tutaenda takribani mikoa saba kwa ajili ya kuonesha mechi mbalimbali kwa hiyo tunawahimiza watumiaji wa kisimbuzi chetu walipie na wale ambao hawana wanunue ili kufurahia burudani,"alisema.

Mechi zitakazoanza kuoneshwa wikiendi hii ni JKT Tanzania dhidi ya Transit Camp na Green Worrioirs dhidi ya Pamba. Tayari kila timu ya championship imeshacheza mizunguko 22 hivyo mizunguko nane iliyobaki ndio itakayooneshwa bure kwa ajili ya kujitangaza.
Mkurugenzi Mwendeshaji wa Tv3 Ramadhan Msemo akizungumza na Wanahabari Leo Machi 24, 2023 mara baada ya Kutangaza rasmi Makubaliano kati ya Tv3 pamoja na bodi ya Ligi Kuu Kuonyesha matangazo ya Ligi ya Championship kwa mechi zilizobakia
Mkurugenzi wa Masomo wa Kampuni ya Startimes David Malisa akizungumza machache mara baada ya kutangazwa rasmi Makubaliano kati ya tv3 na Bodi ya Iigi kuu katika kuhakikisha watazamaji wanalipia Visimbuzi vyao ili kujionea uhondo huo wa ligi hiyo mubashara kuanzia mwanzo hadi mwisho wa ligi hiyo


TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments