Watalaamu kuchambua muswada wa habari

Wataalamu kutoka Umoja wa Wadau wa Kupata Habari (CoRI) kuanzia kesho wanatarajia kuanza kuuchambua muswada wa marekebisho ya Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 ili kuandaa mapendekezo watakayoyapeleka katika Kamati ya Kudumu ya Bunge inayohusika nao kwa hatua zaidi. 

Wataalamu hao wataifanya kazi hiyo baada ya leo wadau masuala ya habari kukutana jijini Dar es Salaam kuangalia kwa kina kilichomo kwenye muswada huo ambao tangu ilipotungwa Sheria hiyo ilisababisha malalamiko ya ukandamizwaji wa uhuru wa habari.

Wadau wa habari wamenakutana wakati ambao Kamati za Kudumu za Bunge zikiendelea na shughuli mbalimbali ikiwa ni maandalizi ya Mkutano wa Bunge unaotarajia kuanza Aprili 4, mwaka huu.


Akizungumza na Mwananchi, Makamu Mwenyekiti wa MISA-Tan, James Marenga amesema Serikali imeshawasilisha bungeni muswada huo hivyo wadau wanapaswa kupeleka mapendekezo yao kwa Kamati ya Bunge inayohusika.

“Serikali imeshatoa mapendekezo yao, sasa ni jukumu letu kuangalia vile vifungu tulivyokuwa tunataka vibadilishwe vimefanyiwa kazi? Kama bado tunatakiwa tupeleke mapendekezo yetu kwa kamati husika na baadaye muswada ukiingia bungeni wabunge wawe na mapendekezo yaliyoshiba na kuamua” amesema

Marenga amesema wadau wa habari waliainisha vifungu zaidi ya 20 vyenye matatizo katika sheria hiyo lakini vilivyofanyiwa kazi havizidi sita na vingi vimelenga kupunguza adhabu.

“Tunaamini tuna fursa kubwa ya kushawishi wabunge watunge sheria bora itakayokuza tansia ya habari, ndiyo maana tunakutana kupata maoni ya wadau halafu watalaamu watachakata maoni hayo kisha tutayafikisha kwa kamati husika” amesema

Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, amesema kuna uwezekano wa kupata sheria nzuri za habari kama wadau watakuwa wamoja na kushirikiana

“Sheria ikiwa nzuri kila mmoja wetu atafurahi, kila sekta itakuwa, naamini bado tuna nafasi ya kujadiliana kwa kina nini kiongozwe au kupunguzwa kwenye muswada wa marekebisho ya sheria ya huduma za habari wa mwaka 2016” amesema Balile.

Mwandishi wa Habari, Hassan Jamal, amesema anaamini kikao kilichofanyika leo kati ya Baraza la Habari Tanzania (MCT) na baadhi ya waandishi wa habari kimetoka na maoni mazuri yatakayosaidia muswada kuboreshwa.

“Wote tusingeweza kwenda kwenye mkutano wa MCT lakini tunatarajia maoni yaliyotolewa na wenzetu yatakuwa mazuri na watalaamu watakaokwenda kuyachakata watatoa mapendekezo mazuri yatakayopelekwa bungeni” amesema

Naye Susan Mbonea, alisema kwa namna muswada ulivyotoka Serikali haijaonyesha dhamira ya kufanya marekebisho yanayolenga kuwapa uhuru waandishi wa habari.

Michael Paul, mwandishi wa kujitegemea amewataka waandishi wa habari kufanya ushawishi kwa wabunge ili waviondoe vifungu visivyofaa mbavyo Serikali haijaviweka kwenye marekebisho.

“Tuandae hoja zetu vizuri na kuonyesha kasoro zilizomo kwenye sheria, tuwaambie wabunge hatuna sababu ya kuvuna na Serikali bali tungependa tuwe na sheria bora isiyoangalia watu, wabunge ni sehemu ya jamii tunayoishi hivyo waandishi wa habari wakiumia wajue nao watapata athari zake” amesema.

Umoja wa Wadau wa Kupata Habari (CoRI) mara baada ya muswada kuwasilishwa bungeni mwezi uliopita ulisema utateua wataalamu ambao watauchambua na kupeleka mapendezo kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge inayohusika kwa hatua zaidi.


TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments