Amesema baada ya kufanyiwa uchambuzi, kamati hizo zitaandika taarifa na kuiwasilisha bungeni katika siku sita za majadiliano kati ya Serikali na Bunge kabla ya kusomwa kwa bajeti kuu ya mwaka 2023/2024.
Novemba mwaka 2022, Bunge liliazimia mambo mbalimbali kuhusu ripoti za CAG kwa mwaka unaoishia Juni 30, 2021 ambayo yalipelekwa serikalini kwa ajili ya utekelezaji.
Akizungumza bungeni jijini Dodoma leo Alhamisi Aprili 20, 2023, Dk Tulia amesema baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa maazimio ya Bunge kuhusu ripoti hiyo, ameielekeza kamati za Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Hesabu za Serikali (PAC) na Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC) kufanya uchambuzi kubaini ni kwa kiasi gani hoja zilizowasilishwa na CAG na kupitishwa kuwa maazimio ya Bunge na kisha kuwasilishwa serikalini zimetekelezwa.
“Ili Bunge lipate mrejesho mzuri naagiza kamati husika mara baada ya kumaliza uchambuzi wake ziandae taarifa ambayo itawasilishwa bungeni wakati wa siku sita za majumuisho ya bajeti kwa mujibu wa kanuni ya 124,” amesema.
Amesema ni matumaini yake kuwa utaratibu huo utaliwezesha Bunge kuisimamia serikali kwa kujua ni namna gani imetekeleza maazimio yaliyotolewa Bunge kuhusu taarifa inayotolewa kila mwaka na CAG
“Tutapata nafasi ya sisi wabunge kujua serikali imetekeleza yapi…, yapi inaendelea na utekelezaji na yale ambayo hawajakamilisha utekelezaji wake. Kamati hizi zitaleta taarifa na yale ambayo yatakuwa yametekelezwa na yale ambayo yatakuwa hayajatekelezwa tutajua tuseme nini,” amesema Dk Tulia.
0 Comments