Kampuni binafsi za ulinzi zabainika kumiliki silaha kinyemela

Kampuni tano binafsi za ulinzi Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga zimebainika kumiliki bunduki na risasi kinyume cha sheria.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi amewaambia waandishi wa habari leo Alhamisi Aprili 27, 2023 kuwa Jeshi la Polisi limebaini uhalifu huo baada ya kufanya operesheni maalum ya kushtukiza katika maeneo ya  Shunu, Nyihogo, Malunga, Mhongolo, na Nyasubi wilayani Kahama.

“Oparesheni hiyo ya polisi ilifanyika kwa kufanya ukaguzi wa kushtukiza katika maeneo ya lindo ya makampuni binafsi ya ulinzi katika Wilaya ya Kahama ambapo makampuni hayo yamekutwa yakimiliki bunduki tano kinyume cha kifungu 10 (7) cha sheria ya usimamizi na udhibiti wa silaha na risasi ya mwaka 2015,” amesema Kamanda Magomi.


Ametaja bunduki zilizokutwa zikimilikiwa kinyume cha sheria na makampuni hayo kuwa ni aina ya Mark IV iliyokutwa na risasi nne, Mark IV iliyokutwa na risasi tatu, Mark IV iliyokutwa na risasi moja, Mark IV iliyokuwa na mbili na Short Gun iliyokutwa na risasi moja.

Katika hatua nyingine, Kamanda Magoma amesema Jeshi hilo limefanikiwa kunasa mali kadhaa zinazoaminika kuwa za wizi ikiwemo magodoro, simu za kiganjani, kompyuta, mitungi ya gesi, Runinga na pikipiki sita.

Jeshi hilo limefanikiwa kuwatia mbaroni watuhumiwa 132 kwa makosa mbalimba yakiwemo ulawiti, ukatili na unyanyasaji kijinsia, mimba kwa wanafunzi na ubakaji.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments