Kawaida aitwisha zigo Wizara ya Kilimo

Wakati Wizara ya Kilimo ikitekeleza mradi wa Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT), Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana CCM (UVCCM), Mohammed Kawaida amesema chochote kitakachokwama lawama ataitupia wizara hiyo.

Aidha kawaida amesema Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imetoa fedha nyingi kugharamia sekta ya kilimo na jukumu la wizara hiyo ni kutekeleza.

Kawaida ametoa kauli hiyo leo, Jumatano Aprili 19, 2023 akihutubia vijana baada ya kutembelea mradi wa BBT Kituo cha Chuo cha Taifa cha Sukari wilayani Kilombero Mkoa wa Morogoro.


"Wizara ya Kilimo imepewa imani kubwa kwa ajenda ya 10/30 (sekta ya kilimo kukua kwa asilimia 10 inapofika mwaka 2030), mradi wa BBT na mambo mengine lukuki," amesema.

Kwa sababu ya imani iliyopewa wizara hiyo, amesema chochote kikikwama UVCCM na vijana wengine watailaumu Wizara ya Kilimo kwa kushindwa kutekeleza.

"Chochote kikikwama UVCCM na vijana wengine Tanzania tutakayemlaumu ni Wizara ya Kilimo na sio Rais Samia, kwa sababu yeye ametoa fedha nyingi katika Wizara hiyo," ameeleza.

Kauli hiyo ya Kawaida ni kama inapigia msumari wa kile kilichowahi kuelezwa na Rais Samia kuhusu mradi wa BBT, kwamba hataki kusikia umekwama.

"Sitaki kusikia tumeshindwa, hakuna kushindwa lazima twende na lazima tufanikiwe,” alisema Rais Samia Machi 20, 2023 wakati wa uzinduzi wa mradi huo.

Onyo hilo liliambatana na onyo kwa Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alipomwambia: “Nataka kuwaambia nimekusudia kwenye hili na sitavumilia Bashe na wenzio pale nitakapotoa fedha za wavuja jasho wa Tanzania ziende kwenye matumizi ya kilimo zikazalishe na fedha ile ikachezewe, sitavumilia,” alisema.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments