Kesi ya diwani wa CCM yachukua sura mpya

Kesi ya diwani wa Ruvu Remit wilayani Simanjiro mkoani Manyara kwa tiketi ya CCM, Yohana Maitei maarufu 'Kadogoo' na wenzake tisa wanaokabiliwa na shataka la kuliharibu kwa mawe gari la CCM imechukua sura mpya baada kuongezewa shtaka jingine.

Hata hivyo, shtaka hilo la kutishia kwa maneno kumuua Isaya Tikoine litawakabili washtakiwa wanane; Williams Yohana (36), Alamayani Kalusu (41), Petro Parkishu (45), Lekiton Olonyokie (65), John Abraham (42), Yohana Pakasi (53), Steve Sasin (69) na Stephen Magirinai (69).

Washtakiwa hao wanane wakazi wa kijiji cha Lerumo kata ya Ruvu Remit, wamesomewa shtaka hilo katika mahakama ya Wilaya ya Simanjiro na mwendesha mashtaka Mosses Hamilton jana Ijumaa Aprili 14, 2023.


Hamilton akisoma shtaka hilo mbele ya hakimu Charles Uiso, amesema washtakiwa hao walifanya kosa hilo Februari 23, 2023 katika kijiji cha Lerumo.

Baada ya kusomewa mashtaka yao waliyakana na kesi hiyo kuahirishwa hadi Mei 10,  2023 itakapotajwa tena mahakamani hapo.

Matei bado anashtakiwa kwa kosa la kuharibu kwa kulishambulia kwa mawe gari la CCM, tukio lililofanyika kijiji cha Lerumo kata ya Ruvu Remit.

Washtakiwa 10 walisomewa shtaka hilo la kushambulia gari hilo mali ya CCM, wakati likiwa na wasimamizi wa CCM wa uchaguzi wa marudio ya mwenyekiti wa kijiji cha Lerumo. 

Hamilton amesema katika kesi hiyo washtakiwa hao 10 wanadaiwa kufanya kosa hilo Februari 23, 2023 wakiwa kwenye kijiji cha Lerumo kata ya Ruvu Remit.

Amedai kuwa washtakiwa hao waliharibu kwa kulishambulia gari aina ya Land Cruser mali ya CCM kwa kulipiga mawe na kusababisha uharibu uliogharimu Sh720,000.

Ametaja maeneo ambayo washtakiwa hao walishambulia gari hilo ni kioo cha mbele na vioo vya pembeni ila hakuna mtu yeyote aliyejeruhiwa kwenye tukio hilo.


Washtakiwa hao waliachiwa kwa dhamana ya kila huku wakikataa kuhusika na tukio hilo.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments