Kikwete awapa jukumu wananchi kumuombea Rais Samia

Rais mstaafu Jakaya Kikwete ametoa rai kwa Watanzania kumuombea Rais Samia Suluhu Hassan ili aendelee kuwa na afya njema na kuwatumikia wananchi kwa kutatua changamoto zinazowakabili.

Kikwete ametoa kauli hiyo  Mjini Kibaha jana Jumatano Aprili 12, 2023 wakati wa kupata futari iliyoandaliwa na Rais Samia  kwa ajili ya wananchi wa Mkoa wa Pwani.

"Kazi aliyonayo Rais ni kubwa, inahitaji hekima na juhudi nyingi hivyo ili kufikia malengo anapaswa kuongozwa na Mungu sisi sote ni vyema tukamuombea,” amesema.
Kuhusu Mkoa wa Pwani, Kikwete amempongeza Mkuu wa Mkoa huo Abubakari Kunenge akieleza kuwa juhudi ambazo amekuwa akizifanya zimesaidia kupiga hatua na kuwapunguzia changamoto wananchi.


"Ni vyema nikakupa sifa zako wakati bado upo, nisisubiri utoke ndipo niseme kazi tunafanya na zimefanikisha kuwapunguzia wananchi kero. Hivyo endelea na juhudi hizo kwani kufanya hivyo unamsaidia Rais," amesema.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge amewataka wazazi nawalezi mkoani humo kuongeza juhudi za kuwalea watoto kwa kuzingatia maadili ili kuleta kizazi chenye tija ndani ya jamii.

"Tukiwapenda zaidi watoto wetu na tukashindwa kuwakemea ili waachane na vitendo viovu tutakuwa tunatenda dhambi ambazo zitatugharimu,"amesema.

Shehe Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Khamisi Mtupa amewatahadharisha baadhi ya watu wanaoomba misaada kutoka maeneo mbalimbali kwa kisingizio cha kuwasaidia watoto yatima kisha wanajinufaisha wenyewe akisema kuwa kufanya hivyo ni sawa na kujiwashia moto kwenye matumbo yao.

"Niwatahadharishe wale mabingwa wa kuandaa maandiko wakiomba msaada kutoka kwenye taasisi za ndani na nje wakidai kuwa wanaenda kuwasaidia yatima kumbe wanajitajirisha siku ya mwisho watambue kuwa watakuwa na húkumu inayowangija," amesema.


Naye  Mwenyeki wa Baraza la Wanawake wa Kiislamu Mkoa wa Pwani, ( Juwakita), Subira Majengo amesema kitendo alichokifanya Rais Samia kwa kutoa futari kwa wakazi wa ndani ya mkoa huo kinaonyesha hali ya upendo kwa wananchi anaowaongoza. Hivyo kuna umuhimu wa kumuombea kwa Mungu ili aendelee na afya njema kwa ajili ya kuwatumikia Watanzania wote.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments