Kingu alalama bei ya saruji kuumiza wananchi

Mbunge wa Singida Magharibi, Elibariki Kingu (CCM) amesema kuna wakati wabunge wanapitisha vitu ambavyo hawavijui lakini vinaumiza wananchi.

Kingu alisema ipo haja ya Taifa kufanya uamuzi mgumu ili kuwasaidia wananchi wanaoumizwa na bei za bidhaa mbalimbali, ikiwamo saruji.

 Kingu alisema hayo alipokuwa akichangia mjadala wa hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zake bungeni jijini Dodoma jana.


Alisema Desemba 7, 2020, Waziri Mkuu alitoa maelekezo ya kuangalia namna gani Serikali itakwenda kusaidia kupunguza makali hayo baada ya kubaini bei za vifaa vya ujenzi, ikiwamo saruji kuwa juu.

 Alisema kuna stadi iliyofanywa na vijana wazalendo wa Tanzania, ilibaini kuwa mpango wa ununuzi wa hisa za kiwanda cha saruji cha Tanga ulikuwa unakwenda kuumiza mfumo wote wa upangaji wa bei ya saruji nchini.

 "Stadi imeonyesha gharama ya kuzalisha mfuko mmoja wa saruji ni Sh5,700 na kampuni ikiachwa, inabidi iuze saruji mfuko mmoja Sh8,700 hadi Sh9,000, lakini wanaumiza wananchi," alisema Kingu.

 Alisema sheria ya ushindani iliyotungwa na Bunge inapaswa kuangaliwa na kulindwa, vinginevyo Watanzania wakigeuka kushoto 'wanapigwa.'

 Alisema umoja wa wazalisha saruji wa Afrika Mashariki unakaa vikao na kupanga bei za saruji kwa kuwaumiza wananchi.

 "Tulichokifanya kibaya zaidi ni kupandisha bei ya ushuru kwa saruji inayoingia nchini kutoka asilimia 23 hadi 35 wakati wazalishaji wa ndani wanazalisha asilimia tatu pekee ambayo haisaidii wakati sekta ya ujenzi inakua kwa kasi,” alisema Kingu.

 Hata hivyo, mbunge huyo alisema wazalishaji kwa kushirikiana na wasambazaji wanatumia mbinu mbalimbali kunyamazisha sauti za wabunge wanaoonekana kupiga kelele.


Alimtaka Waziri Mkuu kuitisha taarifa hiyo ya wazalendo na kuipitia upya ili kusaidia kushusha bei ya saruji ambayo alisema akifanya hivyo, ifikapo Juni, bei ya saruji itakuwa si zaidi ya Sh9,000 kwa mfuko mmoja.

 Mbunge wa viti maalumu, Salome Makamba alisema kimuundo na kimfumo Serikali imejipanga kuweka mfumo wa kiushindani.

Mbunge wa Mtwara Mjini, Hassan Mtenga (CCM) alisema Tanzania haiwezi kuwa na uchumi imara kama haitaimarisha ulinzi wa viwanda.

 Mtenga alisema ulinzi huo uendane sambamba na kuboresha miundombinu ya barabara na madaraja.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments