MAKAMU WA RAIS ATOA WITO KWA JESHI LA POLISI KUJITATHIMINI KUKABILIANA NA MABADILIKO YA TEKNOLOJIA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa Jeshi la Polisi nchini kujitathmini mara kwa mara ili kuwa tayari kukabiliana na changamoto za nyakati hizi za mabadiliko makubwa kiteknolojia na kiuchumi.


Makamu wa Rais amesema hayo leo tarehe 28 Aprili 2023 wakati wa ufunguzi wa Mradi wa kituo cha Polisi Daraja “A” Gezaulole – Kigamboni mkoani Dar es salaam uliogharimu shilingi milioni 899.

Amesema Jeshi la Polisi linatakiwa kuwa kioo cha jamii katika usimamizi wa sheria hivyo ni vema kusimamia maadili mema, nidhamu kazini na uwajibikaji kwa wananchi.

Makamu wa Rais amewaasa polisi kuwahudumia wananchi kwa staha, kusikiliza kero zao na kuzitafutia ufumbuzi kwa wakati pamoja na kuepukana na lugha za matusi, kejeli na dharau.

Aidha Makamu wa Rais ameliasa Jeshi la Polisi kuongeza jitihada katika kukabiliana na ajali za barabarani hapa nchini.

Amesema ni vyema pia Jeshi la Polisi likaangalia uwezekano wa kutumia TEHAMA na kuweka adhabu kali kwa wanaosababisha ajali pamoja na kuacha kupokea rushwa kutoka kwa madereva na kufumbia macho makosa ambayo kugharimu maisha ya watu wengi.

Makamu wa Rais amesema bado taifa linakabiliwa na changamoto ya ajali ambazo zinasababishwa na madereva kutozingatia sheria za usalama barabarani, ulevi, ubovu wa magari pamoja na wengi wao kutokuwa na sifa za udereva.

Halikadhalika Makamu wa Rais ametoa rai kwa Jeshi la Polisi kujidhatiti vizuri katika eneo la upelelezi kwa kuwajengea uwezo vijana wake kupitia mafunzo zaidi katika vyuo mahiri kwenye masuala ya upelelezi hasa wa kesi za jinai ili kukabiliana na mbinu za kisasa za mitandao ya uhalifu nchini na hata Kimataifa.

Amesema hali hiyo itaondoa malalamiko ya wananchi kuhusu upelelezi wa kesi kuchelewa pamoja na wananchi kubambikiziwa kesi.

Pia Makamu wa Rais ametoa wito wa kuimarishwa mahusiano baina ya Jeshi la Polisi na Wananchi ili kudhibiti uhalifu kwa urahisi.

Amesema Uhusiano mzuri kati ya Jeshi la Polisi na raia utawawezesha wananchi kushirikiana na Polisi kudhibiti uhalifu na pia kuboresha ulinzi shirikishi hivyo ni muhimu kwa Jeshi hilo kuandaa mazingira salama ambayo yatawafanya wananchi kuwa na imani kwamba watasikilizwa, hawatadhalilishwa au kuchukuliwa kama wahalifu.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhandisi Hamad Masauni amesema Jeshi la Polisi halitashindwa kuthibiti uhalifu wowote ikiwemo uvunjifu wa maadili unaojitokeza hivi sasa.

Amesema uzinduzi wa Vituo hivyo ni katika kuadhimisha miaka 59 ya Muungano ambao una lengo la kuimarisha udugu na usalama na hivyo kuwafanya wananchi kufanya shughuli za kiuchumi kwa amani na utulivu.

Awali akitoa taarifa za ujenzi wa kituo hicho Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Ispekta Jenerali Camillius Wambura amesema jeshi hilo limeendelea kuboreshwa ikiwa ni mkakati wa serikali wa kuimarisha na kuboresha miundombinu ya jeshi kwa kuzingatia mabadiliko ya sayansi na teknolojia kwa lengo la kuhakikisha haki za binadamu na utawala bora unadumishwa.

IJP Wambura amesema Jeshi la Polisi litaendelea kutunza rasilimali zilizopo ikiwemo miundombinu ya zamani na inayojengwa kwa sasa kwa mustakbali wa usalama wa nchi. Pia amesema Jeshi hilo litaendelea kutekeleza majukumu yake kwa nidhamu, haki, weledi na uadilifu.

Ameongeza kwamba Jeshi la Polisi litahakikisha linasimamia vema mafanikio ya Muungano kwa kulinda amani na utulivu uliopo.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akikagua Gwaride la Jeshi la Polisi wakati alipowasili katika hafla ya Uzinduzi wa Kituo cha Polisi Daraja A – Wilaya ya Kigamboni leo tarehe 28 Aprili 2023.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akizungumza na Askari wa Jeshi la Polisi wakati akikagua kituo cha polisi Wilaya ya Kigamboni katika hafla  ya uzinduzi wa kituo hicho leo tarehe 28 Aprili 2023. 



Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akikata utepe kuashiria Uzinduzi wa Kituo Uzinduzi wa Kituo cha Polisi Daraja A – Wilaya ya Kigamboni mkoani Dar es salaam leo tarehe 28 Aprili 2023.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akihutubia Viongozi, Maafisa, Askari na Wananchi mbalimbali wakati wa Hafla ya Uzinduzi wa Kituo cha Polisi Daraja A – Wilaya ya Kigamboni leo tarehe 28 Aprili 2023.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments