Masauni aruhusu mabasi yanayolala njiani kuanza safari usiku

Serikali imekubali kuruhusu magari yanayofanya safari zake kupitia Wilaya ya Sikonge kutoka jijini Dar es Salaam kuanza safari zake kati ya saa 9 na 10 usiku ikiwa watapenda.

Kauli hiyo imetolewa bungeni leo Alhamisi April 13, 2023 na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Hamadi Masauni wakati akijibu swali la msingi la mbunge wa Viti Maalumu Taska Mbogo (CCM).

Hata hivyo Waziri amesema kinachowapasa wenye mabasi ni kupeleka maombi ya muda gani wanataka kuanza safari zao ili wakapite Sikonge muda ambao utaruhusiwa badala ya kulala.


Hoja ya mabasi kutaka yasafiri hadi usiku imekuwa ikijadiliwa mara nyingi bungeni na mwishoni mwa wiki iliyopita, Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson alikoleza hoja hiyo akitaka kujua sababu zipi ambazo zinazuia mabasi ya abiria yasisafiri nyakati za usiku.

Kwenye swali la msingi Mbunge huyo amehoji ni lini Serikali itaruhusu mabasi kutolala Sikonge (Tabora) badala yake yaendelee na safari zao kwa mikoa mingine.

“Mheshimiwa Spika, wamiliki wa mabasi wanatakiwa kuomba kibali cha kuanza safari zao kati ya saa 9 na saa 10 alfajili ili wakapite mapema Sikonge na kwa kusema hivyo hakutakuwa na zuio la vibali hivyo,” amesema Masauni.

Waziri alisema kipande cha kilomita 161 kutoka Sikonge kwenye eneo lingine kwa muda mrefu kilikuwa na usalama mdogo kwa watumiaji wa barabara hiyo lakini kwa sasa wataliangalia.

Kwa mujibu wa Waziri, tayari Wizara ya Mambo ya Ndani imeshakaa na wadau wengine ikiwemo Wizara ya Uchukuzi na vikosi vingine kwa ajili ya kuweka mazingira mazuri ya kuruhusu mabasi yaanze safari zake usiku.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments