Mbowe amjibu Sanga mbio za urais 2025

Kufuatia kauli ya mbunge wa Makambako, Deo Sanga ya kuitaka Chadema kutosimamisha mgombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, Mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe amesema watasimamisha wagombea ngazi zote kwa kuwa bado wanapambana na CCM.

Mbali na ombi la Chadema kutosimamisha mgombea urais kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2025, Sanga pia alimwomba Mbowe na chama chake kutoa msamaha kwa wabunge 19 wa viti maalumu.

Sanga (CCM) alitoa ombi hilo kwa Chadema bungeni jijini Dodoma juzi wakati akichangia hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi kwa mwaka wa Fedha 2023/23, huku akisema Mbowe hawezi kukataa maombi yake.


Sanga ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Njombe alitoa sababu za kutosimamisha mgombea kwenye nafasi hiyo ya juu akisema inatokana na namna ambavyo amekuwa akifanya Kazi nzuri na Rais Samia Suluhu Hassan katika mambo ya maridhiano.

“Ombi langu kwa Mbowe, kwa sababu anataka kuwafanyia maendeleo Watanzania na mama ameshafanya kazi kubwa dunia inamwelewa, 2025 Mbowe tulia mwachie mama.

“2025 Mbowe shiriki na wabunge, shiriki na madiwani, nafasi ya urais mwachie mama,” alisema.

Kuhusu wabunge 19 wa viti maalumu waliofukuzwa Chadema, Sanga alisema, "Mbowe alishasamehe, naomba asamehe zaidi na hawa wabunge 19 na mmoja wa wajimbo atangaze msamaha pia ili afungue ukurasa mpya, kwenye Urais amwachie mama aendelee bila kusimamisha mgombea."

Akizungumza jana kwa simu na Mwananchi, Mbowe alisema Chadema haipo kwa ajili ya kumbeba Rais Samia.

"Sipendi sana kucomment in person kuhusu Sanga, lakini Chadema haipo kwa ajili ya kumbeba Rais Samia, atabebwa na chama chake (CCM). Tutapambama na Chadema kitakuwa na wagombea wa urais wazuri sina wasiwasi na hilo.

"Useme tumwachia Rais Samia….kwamba kuruhusu mikutano ya hadhara ambayo ipo kikatiba lakini iliporwa kwa miaka saba yaani tumsifu kwa sababu hiyo?”


Mbowe alisema suala la kufutwa kwa kesi iliyokuwa ikimkabili haikuwa fadhila, bali ni wajibu.

"Mama Samia kuruhusu mikutano ya hadhara na kukubaliana na mchakato wa Katiba, huu ni wajibu wake amechelewa kuufanya hatuwezi kumpongeza kwa hilo.Sheria ya mitandao na vyombo vya habari bado changamoto kwa hiyo nchi haiendeshwi kwa hisani ya Rais kwa taasisi na mifumo imara

"Sasa viongozi kama kina Sanga ndio wapambe au tunawaita chawa, kama Rais Samia ni kiongozi imara tutamjaribu katika utumishi wake," alisema Mbowe.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments