MICHEZO YA MEI MOSI 2023 KUFUNGULIWA RASMI MKOANI MOROGORO

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Fatuma Mwasa anatajiwa kuzindua rasmi Michezo ya Kombe la Mei Mosi, Apili 20, 2023 inayofanyika Manispaa ya Morogoro inayowashirikisha wafanyakazi wa umma na sekta binafsi.

Akiongea na Waandishi wa Habari mkoani humo, Mwenyekiti wa Kamati ya Michezo ya Mei Mosi Taifa, ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kondoa Dkt. Khamis Mkanachi amesema mashindano hayo yanatarajiwa kufunguliwa rami na Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Fatuma Mwasa.

“Tuna takriban timu 33 zinazoshiriki Michezo ya Mei Mosi 2023 hapa mkoani Morogoro, mashindano haya yameanza tangu Aprili 16, 2023 na yanategemewa kuhitimishwa Aprili 29, 2023, kabla ya siku ya kilele cha sherehe za wafanyakazi” amesema Dkt. Mkanachi.

Dkt. Mkanachi amesema kuwa awali mashindano hayo yalikuwa yakishereheshwa na vilabu vikubwa nchini vya Simba na Yanga na baadae ilikubalika mashindano hayo yashereheshwe na wafanyakazi wenyewe.

Hatua hiyo imepelekea mashirikisho ya SHIMIWI linaloshirikisha Wizara na Idara za Serikali, SHIMUTA linahusisha mashirika ya Umma, taasisi na makampuni binafsi, SHIMISEMITA linalohusisha Serikali za Mitaa na BAMATA linalohusisha majeshi ya Ulinzi na Usalama.

“Mashirikisho haya yote manne yaliunganishwa kwa pamoja na kuunda Kamati ya Mei Mosi, ukiangalia hapa michezo inayoshindaniwa hapa ni timu zinazotoka katika mashirikisho yote manne ambayo yalianzishwa na Serikali ya Awamu ya Kwanza na Hayati Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere mwaka 1967 mpaka sasa tunaendelea nayo” Dkt. Mkanachi.

Michezo hiyo imefikia siku ya nne ambapo michezo iliyochezwa Aprili 19 ni kamba wanaume na wanawake, mpira wa miguu, mpira wa wavu wanaume na wanawake pamoja na mchezo wa netiboli.

Katika mchezo wa mpira wa miguu, timu ya Maliasili imewafunga Morogoro DC 3-0, TANESCO imewafunga Ukaguzi 7-0, Wizara ya Mambo ya Ndani imewafunga 21st Century 3-0, Hazina imewafunga Ushirika 1-0, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imewafunga Ulinzi 1-0, TPDC wametoka sare na RAS Dodoma 1-1, CRDB wamewatandika TANROAD 2-1, Mawasiliano ikawafunga NFRA 1-0 huku TAMISEMI ikiwaadhibu Wizara ya Kilimo 5-0.

Kwa upande wa mchezo wa netiboli timu ya Uchukuzi imewafunga timu ya Ukaguzi 33-17, TRA imewafunga Morogoro DC 45-6, TANROADS wamefungana na NFRA 17-17, Ulinzi imewafunga CRDB 67-6, Ikulu imewafunga TPDC 42-16, Wizara ya Afya imewafunga Utumishi 27-25, timu ya Mawasiliano imewafunga Mahakama 20-18 na TANESCO wamewafunga Maliasili 35-23.

Mchezo wa kamaba wanaume, timu ya Ofisi ya Rais Ikulu imewavuta timu ya RAS Dodoma kwa mivuto 2-0, Mahakama imewavuta timu ya Wizara ya Kilimo kwa mivuto 2-0, TANROADS imewavuta timu ya Utamaduni kwa mivuto 2-0, TPDC imewavuta timu ya Ushirika kwa m
ivuto 2-0, Mawasiliano wametoka sare na Wizara ya Afya 1-1 na Wizara ya Maliasili imewavuta timu ya Ocean Road kwa mivuto 2-0 wakati kwa upande wa kamba wanawake, timu ya Mahakama imewavuta timu ya Wizara ya Madini kwa mivuto 2-0, Uchukuzi imewavuta timu ya Hazina kwa mivuto 2-0, TPDC imewavuta timu ya Wizara ya Afya kwa mvuto 1-0, Maliasili wamewavuta timu ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa mvuto 1-0.

Pia mchezo wa wavu kwa mara ya kwanza umeingia kwenye mashindano ya Mei Mosi mwaka huu ambapo kwa upande wa wanaume, timu ya Wizara ya Mambo ya Ndani imewafunga Uchukuzi kwa seti 2-0 na TANESCO imewafunga Ushirika kwa seti 2-0 wakati kwa upande wa wanawake TANESCO imewafunga Gairo DC kwa seti 2-0 na Uchukuzi imewafunga TPDC kwa seti 2-0.

Michezo ya Mei Mosi mwaka huu inayowahusisha watumishi wa umma na sekta binafsi inapambwa na kaulimbiu “Miaka Miwili ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Imeimarisha Michezo na Kuongeza Ufanisi Kazini, Kazi Iendelee”.Post a Comment

0 Comments