MIRADI YA BILIONI 1.448 YAFUGULIWA NA KUWEKEWA MAWE YA MSINGI NA MWENGE WA UHURU TUNDURU

MWENGE wa Uhuru umeanza mbio zake mkoani Ruvuma kwa kukagua na kuweka mawe ya msingi katika miradi yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 1.448 wilayani Tunduru.


Miradi iliyowekewa mawe ya msingi ni ujenzi wa mradi wa maji safi na salama katika Kijiji cha Muhuwesi ambao hadi sasa umegharimu zaidi ya shilingi milioni 175 na mradi wa jengo la dharura(EMD) katika hospitali ya wilaya ya Tunduru ambao hadi sasa umetumia zaidi ya shilingi milioni 334.

Miradi mingine ni mradi wa ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa ya TEHAMA na samani zake unaogharimu zaidi ya shilingi milioni 899 na mradi wa madarasa mawili katika shule ya msingi Nandembo wenye thamani ya shilingi milioni 40.

Akitoa taarifa ya mradi wa maji Muhuwesi kwa kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2023,Meneja wa RUWASA wilaya ya Tunduru Mhandisi Maua Mgallah amesema mradi huo ulioanza kutekelezwa Mei 26,2022 unatarajia kukamilika Aprili 30,2023.

Amesema utekelezaji wa mradi huo hadi sasa umefikia zaidi ya asilimia 90 na kwamba utakapokamilika kwa asilimia 100 utahudumia wakazi wapatao 7494 waliopo katika Kijiji cha Muhuwesi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Tunduru Chiza Marando akitoa taarifa ya mradi wa jengo la dharura EMD katika hospitali ya wilaya ya Tunduru,amesema mradi ulianza kutekelezwa Februari 25,2022 na kwamba hadi sasa umefikia asilimia 95 na kwamba unatarajia kukamilika Aprili 30,2023.

“Kukamilika kwa mradi huu kutasaidia azma ya serikali ya kutoa huduma bora za afya kwa wananchi wake na kwamba Tunduru ina barabara kuu ya Mtwara korido kwa kuwa kuna wagonjwa wengi wa kawaida na wanaopata ajali wataweza kupata huduma hivyo kupunguza rufaa za matibabu kwa wagonjwa’’,alisisitiza Marando.

Akizungumza kwa nyakati tofauti wakati anaweka mawe ya msingi kwenye miradi hiyo ,Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Ndugu Abdalah Shaib Kaim ameupongeza uongozi wa wilaya ya Mbinga kwa usimamizi mzuri wa miradi.

Hata hivyo Shaib ameagiza miradi yote kukamilika kwa asilimia 100 kama ilivyoelezwa kwenye taarifa ili wananchi waanze kunufaika na miradi hiyo ambayo serikali imetoa fedha nyingi za kuhakikisha miradi inatekelezwa na kumaliza kero kwa wananchi.

Katika hatua nyingine kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa amefungua miradi ya ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa vyenye thamani ya shilingi milioni 40 katika shule ya msingi Nandembo na mradi wa ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa ya TEHAMA na samani zake vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 899 katika sekondari ya Kiuma.

Mwenge wa Uhuru umeanza mbio zake mkoani Ruvuma kuanzia Aprili 17,2023 na unatarajia kukamilisha mbio hizo Aprili 25,2023 ambapo utakabidhiwa katika Mkoa wa Njombe.

Akizungumza kwenye makabidhiano ya Mwenge wa Uhuru kati ya Mkoa wa Lindi na Ruvuma,Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Ndugu Stephen Ndaki amesema ukiwa mkoani Ruvuma Mwenge wa uhuru utatembelea miradi 61 yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 16.

mradi wa ujenzi wa madarasa mawili ya shule ya msingi Nandembo wilayani Tunduru ambayo yamegharimu shilingi milioni 40,Mwenge wa uhuru umefungua madarasa hayo--

 Mradi wa maji wa kijiji cha Muhuwesi wilayani Tunduru ambao umewekewa jiwe la msingi na Mwenge wa Uhuru 2023,mradi huo ambao utekelezaji wake umefikia asilimia 90,umegharimu shilingi milioni 175 na unatarajia kukamilika Aprili 30 mwaka huu

Katibu Tawala Mkoa wa Lindi Ndugu Zuena Omari Jiri akimkabidhi Mwenge wa Uhuru kushoto Katibu Tawala Mkoa wa Ruvuma Ndugu Stephen Ndaki katika mabidhiano ya Mwenge huo ambao umeanza mbio zake mkoani Ruvuma kuanzia Aprili 17,2023 hadi Aprili 25,2023 utakapokabidhiwa katika mkoa wa Njombe,makabidhiano hayo yamefanyika katika kijiji cha Sautimoja wilayani Tunduru


mradi wa ujenzi jengo la dharura EMD katika hospitali ya wilaya ya Tunduru ambapo serikali imetoa hadi sasa shilingi milioni 334 kwa ajili ya ujenzi na vifaa vya kisasa ambavyo tayari vimefungwa katika hospitali hiyo

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments