Mmomonyoko wa maadili watajwa chanzo cha ukatili

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu kwa kushirikiana na Taasisi ya kijamii inayoshughulikia maendeleo, ukatili wa kijinsia (FAGDI), imesema ukatili unaoendelea kwenye jamii kwa sasa unasababishwa na mmomonyoko wa maadili.

Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dk John Jingu amesema ukatili wa kijinsia hususani kwa watoto unatekelezwa na watu wasio na maadili waliopo kwenye jamii pamoja na hali ya umasikini.

“Vitendo vya ukatili ni uhalifu na sheria zetu zina haramisha hususan kwa watoto. Bahati mbaya tumekuwa tukishuhudia vitendo hivi vinaendelea kutokea kwenye jamii yetu. Kupitia kampeni hii inatukumbusha jukumu la kupambana na aina yeyote ya ukatili,” amesema Jingu.


Jingu ameyabainisha hayo Aprili 28, 2023 katika uzinduzi wa tamasha la kitaifa la kutoa huduma na kutangaza shughuli za maendeleo (TDF), lililofanyika viwanja vya Leaders jijini Dar es Salaam lenye lengo la kuwajengea uelewa wananchi juu ya ukatili wa kijinsia

Balozi wa taasisi ya FADGI, Khadija Kopa amesema matukio ya ukatili yameongezeka hasa kwa watoto. Kwa kushirikiana na Serikali wanakemea vitendo hivyo viovu vinavyofanywa na watu wenye nia mbaya.

Mmoja wa washiriki wa tamasha hilo Saada Abdallah amesema wazazi wanajukumu la kuwakagua watoto mara kwa mara ili kutambua kama wamefanyiwa ukatili kwaajili ya kuchukuliwa hatua za kisheria.

“Usiogope hata kama ni mumeo au hata ni jirani yako kwamba kesho atakunyima chumvi kama amefanya unyanyasaji chukua sheria ili tusaidiane kutokomeza vitendo hivi. Tukisema tufumbie macho havitaisha,” amesema Abdallah.

Naye Shumbana Msabaha mshiriki wa tamasha hilo ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha tatu shule ya sekondari Hananasi, amesema serikali isisite kuchukua hatua kali kwa wale wanaofanya vitendo vya ukatili.


“Wafungwe kifungo cha maisha au adhabu yeyote kali ili watu wengine wenye nia kama hio waogope na kuacha kabisa,” amesema Shumbana.

Tamasha hilo lenye kauli mbiu isemayo Zifiukuki, ‘zijue fursa imarisha uchumi kata ukatili kazi iendelee’ limezinduliwa leo jijini Dar es Salaam na baadae kuendelea kwenye mikoa ya Mwanza, Geita, Kagera, Kigoma, Mara, Songwe, Tanga, Rukwa, na Tabora.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments