Mufti wa Tanzania aiomba Serikali kununua chombo cha kutazamia mwezi

Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir amekemea ufisadi, akihimiza jamii kulinda maadili, umoja na mshikamano, huku akiwaomba viongozi wa Serikali na wadau kusaidia upatikanaji wa darubini ya kukusanya taarifa za mwandamo wa mwezi ili kuimarisha uhakika wa taarifa.

Mwezi mtukufu wa Ramadhani ni kipindi ambacho waumini wa Kiislamu duniani hufunga kwa siku 30 kabla ya kusherehekea siku hiyo kupitia taarifa rasmi ya mwandamo wa mwezi huo.

Hata hivyo, kabla ya kusherehekea, kifaa hicho (moon sighting machine) ndio hutumika kupata uhakika wa mwandamo wa mwezi huo kiimani ili kuondoa utata au mabishano miongoni mwa waumini hao.  


Sheikh Zubeir amesema hayo leo Jumanne Aprili 22, 2023 katika swala ya Eid El- Fitr iliyofanyika kitaifa katika msikiti wa Mfalme Mohamed VI uliopo Wilaya ya Kinondoni, jijini hapa, ikihudhuriwa na Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, mabalozi, mawaziri na watu mashuhuri. 

 “Tunashukuru mabalozi, mawaziri na watu wenye uwezo mliopo hapa, kuna chombo tunakihitaji cha kutazamia mwezi.

“Wenzetu Kenya na Zanzibar wanavyo vifaa hivi, kwa hiyo na sisi tunaomba juu ya jambo hili mtusaidie kunyoosha mkono ili kufanikisha,” amesema Mufti wakati akifunga hotuba yake.

Kwa mujibu wa Bakwata, Tanzania kupitia Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) imekuwa ikikusanya taarifa hizo kwa kushirikiana na mataifa ya Kenya na Zanzibar zinazoendana pia na taarifa za Saudia Arabia na mataifa mengineyo duniani.

Katika hotuba hiyo Sheikh Zubeir ameombea utulivu wa amani nchini. “Pia utuondoshee ufisadi, atuondoshee maadili mabaya kwa vijana wetu na aendelee kumuhifadhi Rais wetu mama Samia Suluhu Hassan pamoja na viongozi wengine dhidi ya maadui.”

Kabla ya Mufti, Mkurugenzi wa Da'wa na Tabligh Tanzania, Alhaj Sheikh Hassan Said Chizenga ametoa hotuba yake pia iliyosisitiza waslamu wote duniani kuendelea kutenda matendo mema.


TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments