Muswada wa Sheria ya Ndoa bado moto

Serikali kuwasilisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Ndoa bungeni katika bunge la bajeti la mwaka huu.

Hayo yamesemwa leo Jumanne Aprili 25,2023 na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Pauline Gekul wakati akijibu swali la msingi la Mbunge Viti Maalum (CCM), Yustina Arcadius bungeni jijini Dodoma.

Mbunge huyo alitaka kufahamu ni lini Serikali itapeleka bungeni Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 kuhusu ndoa za Utotoni.


Akijibu swali hilo, Pauline amesema Muswada wa Sheria ya Ndoa ulifikishwa kwenye kamati ya Bunge Februari 2021 kufuatia maamuzi ya Mahakama ya Rufani.

Amesema katika kesi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali dhidi Rebecca Gyumi, Rufaa namba 204 ya mwaka 2017 iliyotokana na kesi namba 5 ya mwaka 2016 ya Mahakama Kuu iliyotaka Sheria ya Ndoa ifanyiwe marekebisho ili umri wa mtoto kuingia katika ndoa iwe kuanzia miaka 18.

Amesema kurudishwa kwa muswada huo Serikalini kulifuatia kamati ya Bunge baada ya kupitia iliona upo uhitaji wa kushirikisha wadau wengi zaidi ili kupata maoni zaidi.

“Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeshakusanya maoni kutoka kwa wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa kidini, viongozi wa kimila, viongozi wa vyama vya siasa, wanafunzi, wataalamu wa afya na makundi mbalimbali ya wananchi wakiwemo watu wenye ulemavu,”amesema.

Aidha, amesema Aprili 26, mwaka 2023 Wizara imeaandaa Kongamano la Sheria ya Ndoa litakalofanyika mkoani Dodoma.

“Mara tu baada ya Serikali kukamilisha zoezi hili la mwisho, inatarajia kuwasilisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Ndoa Bungeni katika Bunge hili la bajeti.

Naye Mbunge wa Viti Maalum, Salome Makamba amehoji Serikali ilipata wapi mamlaka ya kukiuka maamuzi ya Mahakama Kuu ya kupeleka muswada huo bungeni na badala yake kwenda kukusanya maoni ya wananchi.

Akijibu swali hilo, Waziri wa Katiba na Sheria Dk Damas Ndumbaro amesema muswada huo uliletwa bungeni baada ya uamuzi mahakama kuu lakini chombo hicho kikataka kwenda kukusanya maoni.

Dk Thea Ntara amehoji Serikali ina mpango gani wa kuondoa dhamana kwa wanaume wanaolawiti na kubaka watoto kwasababu kosa hilo ni sawa na mauaji.

Akijibu swali hilo, Dk Ndumbaro amesema dhamana ni haki ya mtuhumiwa na suala la uamuzi wa dhamana linabaki kwa mahakama.


TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments