Polisi yapiga marufuku magari ya mnadani kubeba abiria


 Siku chache baada ya kutokea ajali iliyoua watu 13 mkoani Ruvuma, Mkuu wa Kitengo cha Usalama Barabarani, Mossi Ndozero amefanya msako ili kubaini malori yanayopakia abiria na mizigo kwa ajili ya kuwasafirisha kwenda minadani.

Ndozero amepiga marufuku usafiri huo kupakia abiria huku akishusha wafanyabishara waliokuwa wamepanda maroli hayo na kuwataka watafute usafiri mwingine rafiki, ikiwamo kukodi gari.

Kuanzia saa 9 usiku baadhi ya malori hayo yamekuwa yakisafirisha wafanyabishara wanaoenda minadani katika vijiji mbalimbali mkoani Iringa.


Ndozero akiwa na askari wengine wa jeshi hilo, walijitega kwenye barabara ya Iringa- Pawaga na  kufanikiwa kubaini maroli hayo ambayo licha ya kupigwa faini, abiria walishushwa na kutakiwa wakodi Coaster.

Kutokana na hali hiyo alipiga marufuku maroli hayo kupakia abiria akiwataka watumie njia nyingine ikiwamo kukodi kosta au haisi, zitakazokuwa zinawapeleka huko.

“Hamjasikia wenzetu wamepoteza maisha huko Ruvuma? Kwanini hilo lisiwe funzo kwenu mpaka tuje kukamatana? Nawaomba sana msitumie malori kusafiri kwenda minadani. Jikusanyeni na mkipakia mizigo basi nyie msafiri na   Hiace au Coaster,’ amesema Ndozero na kuongeza;

“Ukiwa kwenye lori na mizigo, likianguka kupona wewe ni jambo gumu, mizigo itakuangukiwa na itakuwa juu yako. Mnapenda kupoteza maisha kizembe?”

Ndozero alikuwa akiwashusha abiria kwenye mabasi hayo kila anapowaona kisha kuwataka watafute usafiri mwingine huku akipiga faini maroli yaliyowapakia.

Akizungumza na wafanyabiashara kwenye minada iliyofanyika katika vijiji vya Ilolo Mpya, jana Aprili 14, 2023, Ndozero aliwataka kutengeneza umoja utakaowasaidia wawe wanakodi magari ya abiria na kuachana usafiri huo.

“Kwa Iringa sitarajii kuona lori lolote linasafirisha abiria, tena mnakaa na kuning’inia juu ya mizigo bila hofua, hii hapana,” amesema Ndozero.


Awali, Mkuu wa Usalama Barabarani Wilaya ya Iringa, Glory Mtui alisema wataendelea kudhibiti mtindo wa magari hayo kupakia abiria.

Kwa upande wao baadhi ya wafanyabiashara walisema changamoto kubwa wanayokutana nayo ni ugumu wa maisha.

“Ni gharama kubwa kusafirisha mizigo na sisi kukodi gari jingine, hali ya uchumi ipo juu na wakati mwingine huko mnadani unaweza kwenda na usiambulie kuuza ndio maana huwa tunaona tujibane kwenye mizigo,” alisema Joseph Ndelwa, mmoja wa wafanyabishara.

Alisema eneo kama Paswaga linayo magari yanayotoka kijiji kila siku asubuhi kuja mjini na kurejea usiku, jambo ambalo ni gumu kwao kuyapanda.

“Mabasi mengi ya vijijini ratiba zao za kusafiri ni ngumu, wanakuja mjini asubuhi na kurudi jioni kiasi kwamba, kwetu ni ngumu kuyatumia hayo,’ amesema.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments