Rais Samia aahirisha tena sherehe za muungano


Wakati maadhimisho ya miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yakisubiriwa hapo Aprili 26 mwaka huu, Rais Samia Suluhu Hassan ameahirisha sherehe za gwaride na badala ameelekeza kufanyika kwa shughuli za maendeleo katika ngazi za mikoa.

Hii ni mara ya pili tangu Rais Samia aingie madarakani kufuta sherehe hizo na kuelelekeza zifanyike shughuli za kijamii ikiwemo usafi wa mazingira.
Taarifa ya kufutwa kwa sherehe hizo ilitolewa jana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipokuwa akizindua ripoti ya pili ya machapisho ya sensa ya mgawanyo wa idadi ya watu kwa maeneo ya kiutawala na umri, katika ukumbi wa Dk Mohammed Shein, Mkoa wa Kusini Unguja.

Hata hivyo, Majaliwa hakutaja kiasi cha fedha kilichokuwa kimetengwa kwa ajili ya maadhimisho hayo wala mahali kitakakoelekezwa.
“Maelekezo ya Rais ya maadhimisho ya sherehe hizo za Muungano mwaka huu, zitafanyika katika ngazi ya mikoa kwa kufanya shughuli za kijamii, kiuchumi na kaulimbiu itakuwa, “Umoja na mshikamano ndiyo nguzo ya kukuza uchumi wetu.”

Alisema maadhimisho hayo yataanza kufanyika Aprili 17, hadi siku ya kilele Aprili 26 mwaka huu.

Waziri Mkuu alisema katika kipindi hicho, taasisi na mikoa ziendelee na uzinduzi wa miradi ya maendeleo sambamba na shughuli za kijamii, hasa upandaji wa miti, uchangiaji wa damu hospitali na vituo vya afya, usafi wa mazingira na mashindano ya michezo na uandishi wa insha kwa shule za msingi na sekondari nchini.

Pia, katika kipindi hicho, ifanyike kampeni ya kupiga vita unyanyasaji na ukatili wa kijinsia na kampeni ya kupambana na wanaotaka kumomonyoa maadili ya taifa.

Kwa sasa viongozi wa dini wamekuwa wakitumia nyumba za ibada kukemea vitendo vya utovu wa maadili na udhalilishaji hasa watoto. Pia, wabunge wamekuwa mstari wa mbele kuonya na kukemea vitendo hivyo, wakiitaka Serikali kuwa makini na kuchukua hatua.
“Tuendelee kufanya majadiliano maalumu na wazee maarufu na vijana kujua muugano wetu, pia iwepo mijadala na makongamano,” alisema Majaliwa.

Pia, alisema sherehe hizo zitafanywa vizuri kitaifa muungano utakapokamilisha miaka 60. Alitoa rai kwa wahusika wa pande zote mbili kuhakikisha wanasimamia maagizo hayo ya Rais.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments