Sagini: Viongozi tumuenzi Mwalimu Nyerere kwa vitendo

Viongozi nchini Tanzania wametakiwa kuiga mfano wa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa kuweka mbele maslahi ya Taifa katika maamuzi yote yanayohusu jamii.

Akizindua wiki ya kumbukizi ya kuzaliwa Mwalimu Nyerere mjini Butiama leo Aprili 13, 2023, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Jumanne Sagini amewataka viongozi kumenzi Mwasisi huyo wa Taifa kwa kufanya maamuzi yanayolenga siyo tu kulinda maslahi ya umma, bali pia kutatua matatizo ya wananchi.

“Kila viongozi tunapofanya maamuzi tujiulize endapo Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere angekuwa hai angekubaliana nayo. Tuache maigizo na unafiki. Tunapofanya jambo au maamuzi tuzingatie misingi ya uongozi bora aliyotauchia Baba wa Taifa,” amesema Sagini


Amesema wakati wa uhai wake, Mwalimu Nyerere alitanguliza mbele maslahi ya umma, hivyo ni wajibu wa viongozi wa sasa kufuata nyayo hizo.

Akizungumzia mmomonyoko wa maadili, hasa kwa vijana, Sagini amewataka wazazi kuwajibika katika malezi ya watoto kujenga jamii bora.

“Kila mmoja kuanzia wazazi na walezi katika ngazi ya familia na jamii nzima atimize wajibu wa malezi ya watoto kujenga jamii na Taifa lenye ustawi,”amesema Sagini

Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF), Profesa Francis Matambalya ametaja malengo ya maadhimisho hayo ya kila mwaka kuwa ni kuhuisha Falsafa na Fikra za Mwalimu Nyerere kwa makundi yote katika jamii.

“Mwalimu Nyerere hajaenziwa ipasavyo kwa sababu hadi hivi sasa kuna tukio moja tu linalomhusisha ambalo ni siku ya kuzima Mwenge wa Uhuru Oktoba 14 kila mwaka kama kumbukizi ya kifo chake,”

“Tumeamua kuwa na wiki hii ya kumbukizi kuhuisha fikra na falsafa za Nyerere. Kumbukizi hii ya kila mwaka inahusu maisha ya Mwalimu Nyerere,”amesema Profesa Matambalya


Akizungumza katika mdahalo maalum kuhusu kumbukizi ya maisha, falsafa na fikra za Mwalimu Nyerere, Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Juma Chikoka ameitaka jamii na Serikali kuendelea kuyaenzi na kuishi katika misingi ile aliyoamini Mwasisi huyo wa Taifa.

“Mwalimu Nyerere alisisitiza uzalendo katika kila uamuzi; lakini hali ya uzalendo miongoni mwetu Watanzania inaonekana kulegalega.  Mfano mzuri ni taarifa ya hivi karibuni ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) inaoonyesha ubadhirifu wa fedha na mali za umma. Turudi kwenye misingi aliyoasisi Baba wa Taifa ,”amesema Chikoka

Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Moses Kaegele amewataka viongozi waliopo madarakani kuhakikisha wanaacha alama na kumbukumbu chanya wanapomaliza muda wao wa uongozi kama alivyo Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.

Kaegele ameiomba Taasisi ya Mwalimu Nyerere kuanzisha na kutekeleza mchakato kufanikisha soma la uzalendo kuingizwa kwenye mitaala na kuanza kufundishwa katika shule zote nchini.

“Muda umefika somo la uzalendo liingizwe kwenye mitaala na kufundishwa kuanzia darasa la awali hadi elimu ya juu,” ameshauri Mkuu huyo wa Wilaya

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments