SERIKALI KUTUMIA TRILIONI 6.7 KUSAMBAZA UMEME KWENYE VITONGOJI

Waziri wa Nishati, January Makamba amesema Serikali imetenga fedha shilingi Trilioni 6.7 kwa ajili ya miradi ya kusambaza umeme kwenye Vitongoji 36,101 hapa nchini ambavyo havijapata huduma ya umeme.

Makamba amesema hayo wakati wa kujadili taarifa ya Wizara ya Nishati kuhusu utekelezaji wa Miradi ya maendeleo inayotokana na fedha za  mkopo wa ECF kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF), kwa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Jijini Dodoma, Aprili 14, 2023.

"Tanzania Bara ina jumla ya vitongoji 64,760 na kati ya hivyo, 28,659 vimepata umeme kupitia miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali ambapo vitongoji 36,101 bado havijafikiwa na huduma ya umeme," amesema Makamba.

Amefafanua kuwa katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imetenga Shilingi bilioni 100 kupitia mkopo kutoka IMF kwa ajili ya kuanza kutekeleza mradi wa kusambaza umeme kwenye Vitongoji vilivyopo katika Mkoa wa Songwe na Kigoma.

Makamba amesema Wakala amepanga kutumia fedha za IMF, kutekeleza mradi wa kusambaza umeme katika Vijiji 654 vya Mikoa ya Kigoma na Songwe, ambapo kuna jumla ya vitongoji 1,821 ambavyo havifakiwa na miundombinu ya umeme.  

"Uchaguzi wa Mikoa ya Songwe na Kigoma umezingatia hali ya upatikanaji wa Nishati ya umeme uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu kwa mwaka 2020 na kuonyesha kuwa mikoa hiyo ina kiwango cha chini zaidi cha umeme kwa upande wa Tanzania Bara," amesema Makamba.

Waziri Makamba, ameeleza kuwa Mawanda ya mradi kwa Mkoa wa Kigoma ni ujenzi wa njia za umeme wa msongo wa kati zenye urefu wa kilomita 321, ujenzi wa njia ya umeme wa msongo mdogo zenye urefu wa Kilomita 700, kufunga mashineumba 350 na kuunganisha wateja wa awali 7,664 katika vitongoji 350 kati ya 905 ambavyo havijapata umeme.

Pia, amefafanua kuwa Mkoa wa Songwe, Mawanda ya mradi ni ujenzi wa njia za umeme wa msongo wa kati zenye urefu wa kilomita 420, ujenzi wa njia ya umeme wa msongo mdogo zenye urefu wa kilomita 608, kufunga mashineumba 304 na kuunganisha wateja wa awali 6,688 katika vitongoji 304 kati ya 916 ambavyo havijapata umeme.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Mh. Daniel Baran Sillo ameipongeza Wizara ya Nishati kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa utekelezaji wa miradi ya kusambaza umeme katika ngazi ya vitongoji.

Kikao hicho kimehudhuriwa na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, Kamishina wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga, Watendaji mbalimbali kutoka Wizara, Shirika la umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
               
  Waziri wa Nishati, January Makamba akizungumza jambo wakati wa kuwasilisha taarifa ya Wizara ya Nishati kuhusu utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo inayotokana na Fedha za Mkopo wa ECF toka IMF kwa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Jijini Dodoma, Aprili 14, 2023
             
                  
Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Bajeti, Daniel Baran Sillo akiongoza kikao wakati wa kujadili taarifa ya Wizara ya Nishati kuhusu utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo inayotokana na Fedha za Mkopo wa ECF kutoka IMF.
              

 Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felechesmi Mramba, akizungumza jambo wakati wa kujadili taarifa ya Wizara ya Nishati kuhusu utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo inayotokana na Fedha za Mkopo wa ECF kutoka IMF kwa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Jijini Dodoma, Aprili 14, 2023
             

   Wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Bajeti na Watendaji walioshiriki kikao wakati wa kujadili taarifa ya Wizara ya Nishati kuhusu utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo inayotokana na Fedha za Mkopo wa ECF toka IMF.

Na Timotheo Mathayo, Dodoma.Post a Comment

0 Comments