Shule tatu za udereva zafungwa, 13 hatarini

Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro limezifungia shule tatu za udereva kutokana na kutokukidhi vigezo vya kuendeshea mafunzo hayo huku nyingine 13 zikisitishiwa kutoa mafunzo kutokana na mapungufu mbalimbali.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo Aprili 19, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amesema kufungwa kwa shule hizo ni kutokana na operesheni inayoendelea mkoani humo ya ukaguzi wa shule za kufundishia madereva ambapo wamebaini mapungufu mbalimbali.

"Katika ukaguzi ambao tumeufanya shule 25 za udereva zilifanyiwa ukaguzi, kati ya hizo shule 13 zilibainika kuwa na mapungufu mbalimbali na zimessitishwa kutoa mafunzo hadi watakaporekebisha mapungufu na kukaguliwa tena, lakini pia tumezifungia shule 3 kutokana na kutokukidhi vigezo vya kutolea mafunzo,"amesema Maigwa.


Kamanda Maigwa amezitaja shule zilizofungwa  kuwa ni Wide Institute, Shekinah V.T.C na Mennonite Training Centre ambazo zipo katika mkoa huo.

Katika tukio jingine, Kamanda Maigwa amesema Jeshi hilo  limewakamata vinara wanne kwa kusafirisha wahamiaji haramu 19 raia wa Ethiopia waliongia nchini bila kuwa na kibali kwa kupitia njia za panya za Kinjiriko, Wilaya ya Same.

"Jeshi la polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama tumewakamata wahamiaji haramu 19 raia wa Ethiopia kwa kosa la kuingia nchini bila kibali, katika kuwakamata wahamiaji hawa pia tumewakamata watuhumiwa wanne waliokuwa wakisafirisha wahamiaji hawa haramu," amesema.

"Wahamiaji hawa tuliwakamata wakiwa kwenye gari aina ya scania walilokuwa wanalitumia kusafirisha wahamiaji hao na tayari watuhumiwa wote tumewafikisha mahakamani," amesema Kamanda Maigwa.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments