Recent-Post

Spika atoa ‘ruksa’ wabunge kujadili ripoti ya CAG


 Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson ameruhusu wabunge na Watanzania kuijadili Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa namna wanavyoona.

Hata hivyo, Dk Tulia amesema Serikali haitalazimika kujibu chochote kwenye ripoti hiyo kwa sasa hadi mwezi Novemba baada ya Kamati za PAC na LAAC kuwa wamefanyia kazi na kuwapa nafasi watuhumiwa kujitetea.

Spika ametoa kauli hiyo Alhamisi Aprili 13, 2023 wakati akitolea ufafanuzi juu ya michango ya wabunge kuhuru ripoti hiyo ambayo mara kadhaa imeleta mvutano ndani ya Bunge kwenye michango.


Mwanzoni mwa wiki Naibu Spika wa Bunge Mussa Zungu aliufuta mchango wa Mbunge wa Kisesa Luhaga Mpina (CCM) akisema ni mapema kujadili ripoti hiyo akisema kanuni za kibunge haziruhusu kwa wakati huu.

Leo Spika amesema kwa kuwa ripoti imeshawasilishwa mbele ya Bunge, ni haki kuijadili na akazuia wabunge wenye utaratibu wa kusimama na kuwapa taarifa wabunge wenzao wanaochangi kwenye Ripoti ya CAG kuacha mara moja.

Amesema kinachotakiwa ni wabunge kutumia nafasi zao kusema wanachokiona ndani ya ripoti hiyo isipokuwa kama hawaposhi, wana uhuru kutumia muda wao na kusema kama wanavyoweza kufanya hivyo.

Spika Tulia ametaja sababu za Serikali kutokujibu ni kutokana na ukweli kuwa Tanzania inaongozwa kwa misingi ya kisheria ambayo inaruhusu upande unaotuhumiwa kuwa nafasi ya kujitetea kwa kutoa hata vielelezo vyao.

“Kingine ni kwamba, taarifa ile imeshafikishwa kwenye kamati husika na wanaendelea kuzifanyia kazi kuanza sasa lakini pia tunatakiwa kuwaita maofisa masulufu ambao kwa wakati huu wanashughulika na bajeti yetu,” amesema Spika.

Amesema wananchi wana matumaini makubwa na Bunge na kwa hiyo haliwezi kuacha kujadili taarifa hiyo kwa umuhimu wake ili wanaohusika waweze kuchukuliwa hatua za kinidhamu kwa watakaobainika kuhusu na ubadhirifu huo.


Wakati huo Spika ameliambia Bunge kuwa, tayari Serikali imeshapokea taarifa ya maazimio ya wabunge waliyoyatoa kwenye Bunge la Mwezi Novemba 2022 kuhusu Ripoti ya CAG na kwamba anafanya utaratibu wa kuifikisha mbele ya wenyeviti wa kamati husika kwa kuifanyia kazi.

Post a Comment

0 Comments