Sumaye: Tusifurahie Bunge la chama kimoja


 Baada ya Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuonyesha ‘madudu’ ya ubadhirifu wa fedha kwenye maeneo mbalimbali, Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, ameibuka akisema Bunge linapaswa kuwa kali katika kuisimamia na kuishauri Serikali.

Sumaye aliyekuwa Waziri Mkuu kwa muongo mmoja kuanzia mwaka 1995 hadi 2005 katika utawala wa Awamu ya Tatu amesema kwa kawaida hakuna Serikali ya demokrasia inayokataa ushauri wa Bunge.

“Haya mambo yanapojitokeza mara kwa mara lazima tukubali kuna tatizo mahali fulani, kubwa kabisa ni Serikali lakini Bunge nalo halifuatilii,” alisema.


Sumaye anatoa kauli hiyo ikiwa ni takribani wiki mbili zimepita tangu Ripoti za CAG Charles Kichere kwa mwaka 2021/22 zilizowasilishwa bungeni jijini Dodoma.

Katika mahojiano kati ya Sumaye na televisheni ya mtandaoni ya Dar 24, yalijikita katika masuala mbalimbali yanayomhusu Sumaye na ripoti za CAG, alisema;

“Bunge lina kazi kubwa na linatakiwa liwe na ukali zaidi, ndiyo maana tunapenda Bunge lenye vyama mbalimbali kwa sababu ni afya kwa nchi.

“Hiki kitu watu hawakielewi, watu wanafikiri ukiwa na Bunge la chama kimoja, ndio njema, hapana. Ukiwa na Bunge la chama kimoja ndani ya mfumo wa vyama vingi ni tatizo,” alisema.

Ripoti za CAG alizokuwa anadili Sumaye zimeonyesha ubadhirifu katika taasisi na mamlaka za Serikali, hali ambayo imewaibua wadau wakitaka hatua kali zichukuliwe dhidi ya wahusika.

Tayari Rais Samia Suluhu Hassan, amekwishaanza kuchukua hatua kwa kutengua uteuzi wa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ndege za Serikali (TGFA) na kuivunja Bodi ya Shirika la Reli Tanzania (TRC).

Mbali na hilo, Rais Samia ametoa maagizo kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Dk Moses Kusiluka kuhakikisha makatibu wakuu na watendaji wakuu wote wa taasisi za Serikali wanapitia kwa kina taarifa ya CAG, wajibu na kuzifanyia kazi kwa haraka hoja zote.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments