Katika kufanikisha hilo, kila nchi itajenga kituo chake ambacho kitakusanya maofisa kutoka pande zote mbili wanaohusika katika ukaguzi wa watu wanaotaka kuvuka mpaka kwenda nchi nyingine.
Hayo yameleezwa na Meneja wa Wakala wa Barabara Mkoa wa Kigoma, Narcis Choma wakati akizungumzia miradi mbalimbali inayotekelezwa katika mkoa wake ikiwemo ya barabara na maendeleo.
Choma amesema uwepo wa kituo hicho utasaidia kupunguza muda wanaotumia watu katika kufanyiwa ukaguzi pindi wanapotaka kuingia nch nyingine.
"Hii inamaanisha kuwa, mtu akikaguliwa katika kituo chetu cha hapa, upande wa Burundi hawatakuwa na haja ya kumkagua, akikaguliwa katika kituo cha Burundi sisi hatutakuwa na shida naye," amesema Choma.
Amesema kila kituo kitajumuisha maofisa wanaohitajika ikiwemo wale wa uhamiaji, maofisa mapato kutoka nchi zote.
"Kwa upande wetu kituo cha pamoja kitajengwa Manyovu/Mugina na moaka sasa Mhandisi Mshauri ambaye ni Kagga & Partners Ltd kutoka Uganda alishakabidhiwa site tangu Novemba 2, 2020 na tayari ameshawasilisha ripoti ya Mwisho (Final Design Report)," amesema Choma.
Wakati hilo likifanyika baadhi ya wananchi walisema itasaidia kuondoa usumbufu waliokuwa wakikutana nao awali.
"Kukaguliwa mara mbilimbili ni kero, umekaguliwa kule dakika chache baadaye unakaguliwa tena wakati hakuna kilichobadilika, hii itatusaidia kufanya manbo yetu kwa wakati kwa sababu hata utendaji wa maofisa haulingani," amesema Ndayanse Mtweve mkazi wa Manyovu.
Betabula Mganyizi alitaka ujenzi ufanywe haraka ili waweze kufurahia matunda yake.
0 Comments