UVCCM yataka udahili wa vijana BBT uongezeke


 Wakati mradi wa Jenga kesho iliyobora (BBT) ukitarajia kunufaisha vijana milioni tatu kufikia mwaka 2030, Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Mohammed Kawaida ametaka juhudi ziongezwe kuhakikisha idadi ya wanaodahiliwa kila muhula inaongezeka ikilinganishwa na ya sasa.

Kauli hiyo ya Kawaida inatokana na ukweli kwamba, idadi ya waliodahiliwa kwa muhula wa kwanza wa mradi huo unaohusisha miezi minne vijana 812 walidahiliwa kati ya takribani 20,000 walioomba.

Kawaida ametoa kauli hiyo jijini Mbeya leo, Jumanne ya Aprili 18, 2023 alipotembelea Kituo cha mafunzo ya mradi wa BBT Uyole, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi katika Mikoa ya Dodoma, Mbeya, Morogoro, Kilimanjaro, Arusha na Mtwara.


Kwa mujibu wa Kawaida, iwapo katika kila muhula wa miezi minne watakaochaguliwa ni 812, hadi kufikia mwaka 2030 mwisho wa mradi ni vijana 22,736 pekee ndiyo watakaokuwa wamenufaika ambao ni chini ya makusudio.

"Tunalenga kuwanufaisha vijana 200,000 lakini kwa idadi hii ya tunaodahili kwa muhula kuna haja ya kuongeza mbinu ili kwa muhula wadahiliwe wengi zaidi na tufikie lengo," amesema.

Idadi ndogo ya waliodahiliwa katika muhula wa kwanza, unatokana na kile kilichoelezwa na Mratibu wa mradi huo, Vumilia Zikankuba kwamba ni mwanzo wa mradi.

"Siku zote huwezi kuanza mwanzo kwa kukimbia kwa hiyo huu ni mwanzo idadi inatarajiwa kuongezeka," amesema.

Mratibu huyo kutoka Wizara ya Kilimo, amesema kadri muda unavyokwenda idadi ya wanaodahiliwa itaongezeka maradufu.

"Tunatarajia kuchukua vijana mara mbili hadi tatu zaidi ya waliodahiliwa katika muhula wa kwanza," ameeleza.

Vumilia amebainisha kuwa, lengo la mradi huo ni kunufaisha vijana milioni tatu kufikia ukomo wake mwaka 2030.

"Kufikia mwaka 2030 vijana milioni tatu watanufaika na ajira katika mradi huu," amesema mratibu huyo.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments