Waathirika tope la mgodi walipwa fidia Sh1.8 bilioni

Watu 294 kati ya 304 walioathiriwa na matope baada ya bwawa la matope la Mgodi wa Almasi wa Williamson Diamond eneo la Mwadui wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga kupasuka wamelipwa fidia.

Waathiri kutoka vijiji vya Ng'wanholo na Nyenze wamelipwa fidia ya fedha taslim Sh1.8 bilioni, mali na vifaa mbalimbali vilivyosombwa na kuharibiwa wakati wa tukio hilo lililotokea Novemba 7, 2022. 

Akizungumza leo Aprili 15, 2023 wakati wa hafla ya kukabidhi fidia hiyo, Ofisa Mahusiano wa Mgodi wa Mwadui, Bernard Mihayo amesema waathirika hao pia watajengewa nyumba 47 zenye gharama tofauti katika maeneo mapya wanakohamishiwa.

"Waathirika 10 bado hawajalipwa kwa sababu ya mvutano kati yao; watalipwa mara watakapomaliza tofauti miongoni mwao," amesema Mihayo

Pamoja na kufidiwa mali iliyoharibika ikiwemo vyakula, pikipiki, baiskeli, mashine za kuvuta na kuambaza maji na samani za ndani, waathirika hao pia wamepewa vifaa vya ujenzi vikiwemo nondo na mabati.

"Mgodi utaendelea kulipa fidia ya chakula kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza itakuwa mwezi Juni na Julai huku awamu ya pili itatolewa mwezi Oktoba na Novemba," amesema Ofisa huyo

Jonh Makune, mmoja wa waathirika waliopokea fidia ameishukuru Serikali na mgodi wa Mwadui kwa kutekeleza ahadi ya kuwalipa fidia huku akiwaasa waathirika wote kutumia vema fidia walizopewa kuhakikisha familia zao zinarejea katika maisha ya kawaida.

Kauli kama hiyo imetolewa na mwathirika mwingine, Sophia Mathias akisema awali hawakuwa na matumaini ya kulipwa fidia.

"Kwa kweli tunaishukuru Serikali na mgodi kwa kutekeleza ahadi. Hatukuwa na uhakika wa fidia lakini leo ahadi imetimia," amesema Sophia

Pamoja na fidia, Sophia pia ameushukuru uongozi wa mgodi wa Williamson Diamond Mwadui kwa kuwahudumia chakula tangu janga la makazi na mazao yao kuharibiwa lilipotokea.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Ng’wanholo, William Kabisi ameungana na wananchi kuushuru uongozi wa mgodi na Serikali kwa kuwalipa fidia waathirika huku akifichua kuwa hata uongozi wa kijiji nao ulikuwa na mashaka kuhusu ahadi ya kulipa fidia ingetekelezwa.

Kwa kuonyesha furaha na kuthamini jitihada za Ofisa Mahusiano katika kushughulikia suala la fidia kwa waathirika, Mwenyekiti wa kijiji cha Nyenze, Revocatus Kulwa amependekeza eneo ambalo wananchi watajengewa nyuma mpya 47 liitwe Bernad Mihayo kama njia ya kumuenzi.

Ofisa Ardhi Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Grace Mwandu amewaomba waliolipwa fidia kuhakikisha wanaitumia kwa malengo yaliyokusudiwa ambayo ni kupata mahitaji ya msingi ya familia.TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments