Waislamu watakiwa kujiepusha na chuki

Wauminu wa dini ya kiislamu nchini wametakiwa kuendeleza mema yote waliyofanya katika kipindi cha mfungo wa ramadhani na kujisafisha mioyo kuondokana na chuki.

Kauli hiyo imetolewa leo April 22, 2023 na Sheikh Abbas Ramadhani Imamu wa msikiti wa Mtoro uliopo kariakoo Dar es Salaam wakati wa swala ya Eid ul Fitr,

Eid ul-Fitr, ni sikukuu ya kiislamu inayomaliza mwezi wa Ramadan na tayari mataifa mbalimbali yamesherekea sikukuu hiyo jana April 21, 2023 lakini yapo mataifa ikiwamo Tanzania ambayo leo ndio inasherekea siku hiyo.


Akitoa mawaidha baada ya swala ya Ramadhani, Sheikh Ramadhani amesema Waislamu wanapaswa kutafakari funga yao kwa kutenda mambo mema kwenye jamii na kutoa sadaka kwa watu masikini badala ya kuendeleza chuki dhidi ya majirani yao.

"Tengenezeni nafsi zenu ziwe nzuri, kila mtu achunguze moyo wake upo sawa na mwenzake, hakuna ugonjwa mbaya kama kuwa na chuki, usiangalie tu kwamba umefunga je upo sawa na jirani yako," amesema.

Amesema wapo watu walitamani kufikia siku ya leo kumtukuza Mungu lakini hawakupata nafasi hiyo hivyo kila mtu aliyehai anapaswa kutenda yale yanayompendeza Mungu.

Akizungumzia suala la maadili amesema ni muhimu sherehe zote zitakazofanyika ziwe za kumpendeza Mungu akikemea mambo ya uzinzi akisema, husda na fitna zinamuweka mtu mbali na Mungu.

Kwa upande wake Sheikh Othman Hamis amewataka Waislamu kutotumia sikuu ya Eid kutenda maasi kwani funga yao ya siku 30 haitakuwa na màana kwa Mungu.

"Imani zenu zisiishe leo, endelezeni yale mema yote mliyokuwa mnafanya wakati wa mfungo, tumieni siku hizi kwenda kuwaslimia wagonjwa hospitali na msiwasahau maimamu na walimu wa madarasa wana hali mbaya," amesema.

Idriss Shaban mkazi wa Magomeni amesema siku ya leo kwake itakuwa muhimu kutoa sadaka kwa makundi yasiyojiweza.

"Nimeandaa chakula nyumbani nimewaita majirani na watu mbalimbali ambao kupata chakula kwao ni tabu, kwangu hii itakuwa baraka," ameeleza.

Kwa nini waislamu wanafunga

Ramadan au Ramadhani ni mwezi wa tisa katika kalenda ya Kiislamu na mwezi wa kufunga  kuadhimisha ufunuo wa kwanza wa Qur'an kutokana na mafundisho ya Mtume Muhammad.

 Mwezi wa mfungo huwa na siku 29 au 30 kutegemeana na kuonekana kwa mwezi.

Kufunga ni moja ya nguzo tano za uislamu, Mwislamu mwenye afya nzuri, anatakiwa kushiriki katika swaumu ambayo ni ibada ya kufunga chakula na kinywaji mchana kutwa, pamoja na kujizuia kufanya mapenzi toka alfajiri hadi Magharibi.

Matendo hayo ya toba yanaendana na kuswali na kusoma Quran kwa wingi.

Mwisho wa Ramadhani ni sikukuu ya Eid ul Fitr ambayo ni sherehe ya furaha na kupongezana.


TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments