Watalii waongezeka kupanda mlima Kilimanjaro

Uboreshaji wa miundombinu katika Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro (Kinapa), uliofanywa kwa kutumia fedha za afueni ya Uviko-19 na filamu ya Royal Tour vinatajwa kuwa sababu ya kuvutia watalii wengi kupanda mlima huo.

Kutokana na filamu hiyo iliyofanywa na Rais Samia Suluhu, inaelezwa idadi ya watalii wanaopanda mlima huo, imeongezeka kutoka watalii 12,000 mwaka 2020/2021 hadi kufikia watalii 47,000 katika mwaka unaomalizikia wa 2022/2023.

Akizungumza na wanahabari waliotembelea hifadhi hiyo, Kaimu mkuu wa Kinapa, Mapinduzi Boniface, alisema Kinapa kupitia Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa), ilipokea Sh797.7 milioni za ahueni hiyo ya ugonjwa wa Uviko.

Septemba 2021, Tanzania ilipokea mkopo wenye masharti nafuu wa Dola 567.25 milioni sawa na Sh1.291 trilioni kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF) ambazo zilielekezwa sekta afya, elimu, maji na utalii na mazingira.

Boniface ambaye pia ni Afisa Uhifadhi mkuu anayesimamia kitengo cha ulinzi ndani ya Hifadhi ya Kilimanjaro, alisema Sh797.7 milioni ambazo Kinapa ilipatiwa, zimesaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha miundombinu katika mlima Kilimanjaro.

Miradi ambayo ilifadhiliwa na fedha hizo ni pamoja na kutengeneza viwanja vitano vya kutua helkopta (helipad) za uokoaji zinazoendeshwa na kampuni ya Kili Med Air na tayari kampuni nyingine mbili zimepewa mkataba kutoa huduma hiyo.

“Wageni wanapopanda mlima wanapenda kuhakikishiwa usalama wao. Kwa hiyo wakishajua kuna huduma za uhakika za helkopta maana wanajiamini kuwa tukienda Kilimanjaro ni eneo salama tutafanya utalii bila shida,” alisema.

Fedha hizo pia zimetumika kutengeneza njia ya wageni yenye kilometa sita kutoka kituo cha Mweka Hut kwenda millennium na kutengeneza njia ya kilometa nne za kutoka njia ya Horombo kwenda eneo linalojulikana kama Last Water Point.


Mbali na miradi hiyo, pia zimetumika kujenga njia ya wageni kutoka kituo cha Second Cave kwenda Kikelelwa na kutengeneza kingo zinazotumika na wageni kujikinga kutokana na njia wanazopita katika eneo la Gilmans kuelekea Stella.

Pia kumejengwa vivuko kutokea Lava Tower kuelekea Baranco na ujenzi wa barabara ya zege yenye urefu wa kilometa saba kutoka njia ya Kilema kuelekea Horombo, maboresho ambayo yamepongezwa na baadhi ya watalii.

“Toka Rais alipofanya ile filamu ya Royal Tour tumeona kumekuwa na ongezeko la watalii. Kwa mfano kipindi cha 2020/2021 ilikuwa na watalii 12,000 kwa mwaka mzima lakini mwaka huu tunavyoongea wameshafika wageni 47,000,” alisema.

“Tunaamini hili ongezeko la wageni limechangia na impact ya utangazaji wa utalii uliofanywa na Rais mwenyewe lakini kupitia hii miradi imesaidia kuboresha miradi ya utalii mlima Kilimanjaro ambayo imesaidia nchi yetu,”alieleza Boniface.

Mtalii Babra Lewis ambaye ni raia wa Uingereza ambaye alikutwa na wanahabari akishuka mlima huo baada ya kufika kilele cha Uhuru, alisema ameridhishwa na mazingira ya usalama katika mlima huo na kuahidi kuutangaza mlima huo.

Mmoja wa waongoza watalii katika mlima huo, Nicholaus Kiberiti ambaye amefanya kazi hiyo kwa miaka 20, alisema kujengwa kwa maeneo ya kutolea huduma ya uokoaji mlimani, kumefanya hifadhi hiyo kuvutia wageni.

“Ukiacha suala la uokoaji, lakini kwa jinsi njia zilivyotengenezwa na kuboreshwa inasaidia wageni kushuka vizuri bila kuteleza kwa vile njia zimetengenezwa vizuri. Kwa kweli kwa hili naomba nimpongeze sana Rais na Tanapa,”alisema Kiberiti.


Muongoza watalii mwingine Respicius Baitwa ambaye ameshapanda vilele vitano vya milima maarufu duniani alisema kuboreshwa kwa njia za wageni na huduma ya uokoaji kumeufanya mlima huo uzidi kupanda chati kimataifa.


TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments