Akizindua zahanati hiyo leo Aprili 26, 2023 ikiwa ni maadhimisho ya miaka 59 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Christina Mndeme amesema wananchi hao wataondokana na adha ya kwenda kupata matibabu nje ya kata hiyo.
“Ndugu zangu wanamasekelo kabla ya muungano tulikuwa na zahanati 10 kwa mkoa mzima, lakini kwa sasa tuna zahanati 250 hivyo tunatakiwa kuendelea kuiunga mkono Serikali ya awamu ya sita ili iweze kufanya maendeleo makubwa zaidi,”
“Zahanati hii imeletwa hapa kwa ajili ya wananchi, hivyo niwaombe tuitunze tusilete hujuma yeyote, pia niwaombe wananchi wote wa Mkoa wa Shinyanga muendelee kujikinga na Malaria kwani mkoa wetu bado una maambukizi ya Malaria hivyo ni jukumu langu na wewe kuchukua tahadhari kwa kutumia vyandarua tulivyopewa,”amesema Mdeme
Amesema maendeleo yote ya mkoa huo ikiwemo zahanati ya Masekelo yanatekelezwa na ilani ya CCM hivyo huduma zote zitapatikana zikiwemo za mama na mtoto pamoja na huduma za wajawazito.
Katika hatua nyingine, Mdeme amewataka wanafunzi mkoani humo kutoshawishika ili watimize ndoto zao za maisha.
Katibu wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Dornad Magesa amesema Chama hicho kitaendelea kusimamia ilani yake na kuhakikisha Serikali inatekeleza miradi mbalimbali ya kimaendeleo na kuwataka wananchi waendelee kukiamini.
Baadhi ya wananchi wa kata hiyo wameishukuru Serikali kwa kuwajengea zahanati hiyo wakidai walikuwa wakipata shida kwenda kutibiwa katika zahanati za kata zingine lakini kwa sasa watapata matibabu karibu.
0 Comments