CCM yatoa maelekezo sakata la mgomo wafanyabiashara Kariakoo, Katiba Mpya

 Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) leo Jumapili Mei 21, 2023 imeingiza mguu katika sakata la mgomo wa wafanyabiashara Kariakoo huku ikiitaka Serikali kutafuta kiini cha tatizo na kukitafutia ufumbuzi.

Kamati hiyo imetoa maelekezo hayo katika kikao chake maalum kilichoongozwa na Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan baada ya kupokea na kujadili taarifa kuhusu mgogoro wa wafanyabiashara wa soko hilo la kimataifa.

“Kamati Kuu baada ya kujadili imeielekeza Serikali kufanya uchambuzi wa kina wa masuala yaliyoibuliwa na kulalamikiwa na wafanyabiashara wa Kariakoo ili kutafuta kiini cha tatizo halisi na kuyapatia ufumbuzi wa kudumu,”imesema taarifa ya chama hicho iliyotolewa na Katibu wa Halmashauri Kuu Taifa, Itikadi na Uenezi, Sophia Mjema.


Vilevile, Kamati Kuu imeielekeza Serikali kuhakikisha inatengeneza utaratibu wa kutatua changamoto mapema kabla hazijaleta madhara katika jamii kama ilivyokuwa katika mgogoro wa soko la Kariakoo.

Kamati Kuu imetoa maelekezo hayo kwa Serikali ikiwa ni siku nne zipite tangu wafanyabiashara wa soko la Kariakoo wamalize mgomo wao ambao ulifanyika kwa siku tatu mfululizo kwa kufunga maduka yao kushinikiza kutolewa kwa kodi ya stoo na kukomeshwa kwa kile walichokiita kamatakamata inayofanywa na Mamlaka ya Mapato (TRA).

Hata hivyo, mgomo huo ulitamatika baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kufanya vikao viwili na wafanyabiashara hao huku kikao cha kwanza kilichofanyika Mei 15, 2023 kisifue dafu na baadhi ya wafanyabiashara waliendelea na mgomo hivyo kulazimika tena Mei 17, 2023 kufanya kikao kingine cha wazi katika viwanja vya Mnazi Mmoja.

Katika kikao cha pili kilichohudhuriwa na mamia ya wafanyabiashara wa soko hilo maarufu nchini lenye kila aina ya pilikapilika kilifanikisha kumaliza mgogoro huo baada ya Majaliwa pamoja na Waziri wa Fedha na Mipango, Mwigulu Nchemba na Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Ashatu Kijaji kuwasikiliza wafanyabiashara hao wakitema nyongo kuhusu kero zinazowasibu na baadaye kuunda kamati ya watu 14 kushughulikia matatizo hayo ikiwahusisha wafanyabiashara na watumishi wa Serikali.


Kwa upande mwingine, Kamati Kuu imempongeza Rais Samia kwa kuanzisha mchakato wa Katiba Mpya na kukamilisha ujenzi wa Ikulu Mpya ya Chamwino iliyozinduliwa rasmi Jumamosi Mei 20, 2023.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments