Dawa ya mikopo umiza yaja

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dk Dorothy Gwajima amesema wanawake wanaolia kuhusiana na mikopo inayowaumiza watapona baada kuona fursa nyingine kupitia majukwaa ya uwezeshaji kiuchumi wanawake.

wajima amesema hayo leo Alhamis Mei 18, 2023 wakati akihitimisha hoja ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa mwaka 2023/24.

“Wanawake wote wanaolia mikopo isiyoeleweka sasa wanakwenda kupona watakwenda kupata fursa nyingine za mikopo nafuu kupitia majukwa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi,” amesema.


Pia amesema amewataka wanaojihusisha na mikopo inayowaumiza wanawake kwenda kujisajili ili kupata miongozo sahihi ya utoaji wa mikopo.

“Majukwaa yameanza mtaniona hadi kwenye ofisi zenu mniambie kuwa mmesajiliwa na nani, mlipewa kibali na nani cha kuwapatia wanawake hawa mikopo pengine hata haikidhi hadhi ya utoaji mikopo. Waende kujisajili sehemu sahihi waende wapewe miongozo,” amesema.

Aidha, amesema hivi sasa vitambulisho vya wamachinga vitakavyotolewa vitakuwa vya kijiditali na vitawezesha watu hao kutoa fedha na kupokea fedha.

Amesema vitambulisho hivyo vimeunganishwa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) na Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) pamoja na maeneo yote ambayo mmachinga atakuwa anapita kwenye mzunguko wake wa kupata fedha.

“Akionesha kitambulisho wanamsoma, mifumo inasomana. Ni kipindi cha mpito mwaka huu wa fedha, 2023 umekamilika. Tutaanza na ngazi ya mkoa kisha tutakwenda nchi nzima, litawanyanyua wamachinga kuaminika na kupewa mikopo,” amesema.

Kwa upande wa pensheni kwa wazee, Dk Gwajima amesema wanafanya mapitio ya sera ya wazee ya mwaka 2003 ambayo ndani yake watakuja na sheria ya wazee ambayo itakuwa na pensheni pia kwa kundi hilo.


TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments